-

IDF kuanzisha mfuko kusaidia somo la elimu ya dini ya Kiislamu

Baadhi ya viongozi wa Taasisi ya Islamic Development Foundation (IDF) wamezungumzia maboresho ya somo la elimu ya dini ya Kiislamu na kubainisha kuwa taasisi hiyo inatarajia kuanzisha mfuko maalumu wa fedha kwa ajili ya somo hilo.

Tunataka huyu mwanafunzi anayesoma Somo la Elimu ya Kiislamu aweze kuhusianisha somo hilo na masomo mengine,” alisema Sheikh Muhammad

Akiongea na gazeti Imaan kwa njia ya simu, Mratibu wa IDF mkoa wa Tanga, Sheikh Hamis Shemtoi alisema mkakati huo utasaidia kupata fedha kwa ajili ya kulipa posho za baadhi ya walimu wa somo hilo na pia kununua vitabu vya somo hilo la elimu ya dini ya Kiislamu (EDK).

Sheikh Shemtoi aliongeza kuwa, ili kupata fedha za kutunisha mfuko huo, watahamasisha taasisi na wadau mbalimbali kuchangia. Shemtoi alisema, tayari Mufti, Sheikh Abubakar Zubeir ameunga mkono mipango hiyo na kinachofuata ni utekelezaji. Pia, Sheikh Shemtoi alitaja mikakati mingine ni kuendelea kutoa semina kwa walimu na wazazi ili kukuza hamasa ya kufundisha na kulisoma somo hilo.

Sheikh Shemtoi aliongea hayo wakati huu ambapo IDF inaendesha semina maalumu ya wiki moja kwa walimu wa ngazi za shahada na astashahada juu ya kufudisha somo la EDK.

Semina hiyo ambayo ilianza Julai 8 na inatarajia kumalizika Julai 14 mwaka huu, inafanyika katika shule ya Muzdalifah jijini Dar es Salaam chini ya kauli mbiu isemayo: “Somo la elimu ya dini ya Kiislamu shuleni ni nguzo muhimu ya kupata wasomi bora wenye maadili na utayari wa umma kwa maendeleo ya jamii.

Akiongelea zaidi lengo la semina hiyo, Sheikh Shemtoi alisema kuwa semina hiyo imeandaliwa ili kuwapa mafunzo walimu hao juu ya jinsi ya kufundisha EDK katika namna itakayoleta tija kwa mwanafunzi, mhitimu na jamii kwa ujumla.

“Tumeona kuna upungufu kadhaa katika ufundishaji wa somo hilo, hivyo tukaandaa semina hii maalumu ili kuwapa mafunzo walimu na wazazi wajue umuhimu wa somo hilo na mbinu za kulifundisha kwa tija,” alisema Sheikh Shemtoi.

Sheikh Shemtoi aliongeza kuwa, sababu nyingine ya kuandaa semina hiyo kwa walimu ni baada ya kuona wanafunzi wa Kiislamu wanakosa muda wa kusoma madrasa.

“Wanafunzi wengi wa Kiislamu wamekuwa hawana muda wa kusoma madrasa, na hivyo tunaona sasa ni vema walimu wakapewa mbinu ili wanafunzi hao waweze kujifunza dini yao kupitia somo la elimu ya Kiislamu huko huko shuleni,” alisema Sheikh Shemtoi.

Akizungumzia juu ya kuliboresha somo hilo la EDK, Naibu Katibu Mkuu wa IDF, Auni Rastam Khaj alisema kuwa, kumekuwepo na kozi mbalimbali zinazoandaliwa kuboresha ufundishaji wa somo hilo.

Zipo kozi fupi zinazotolewa kwa walimu wa madrasa ili kuwajengea uwezo. Jopo la elimu ya Kiislamu (Islamic Education Panel) limeweka mratibu kila mkoa na kanda ambao wanafundisha katika vyuo vya ualimu,” alisema Khaj.

Naye Mratibu wa IDF mkoa wa Dodoma, Sheikh Twalib Muhammad alisema kuwa, katika semina hiyo walimu wanapewa mbinu za kuwezesha wanafunzi wanaofundishwa EDK kuwa na uwezo wa kuunganisha maarifa ya elimu ya dini na masomo mengine.

“Tunataka huyu mwanafunzi anayesoma Somo la Elimu ya Kiislamu aweze kuhusianisha somo hilo na masomo mengine,” alisema Sheikh Muhammad na kuongeza: “Mathalani mwanafunzi anayesoma Jiografia au Biolojia basi aweze kuhusanisha na elimu iliyomo katika hilo somo la dini ya Kiislamu.”

Pia mratibu huyo alisema, semina hiyo inalenga kuwawezesha walimu kufundisha somo hilo la EDK katika namna ambayo itawajenga wanafunzi kimaadili na kuzalisha wahitimu bora.

Vijana wengi wa Kiislamu wanaomaliza wanakuwa hawana maadili. Mwisho tunasikia masuala ya ufisadi, sasa ndio tunataka somo hilo liwafanye wanafunzi na wahitimu kuwa na maadili na kuitumikia jamii vema,” alisema mratibu huyo. Mratibu huyo pia alisema kuwa, semina hiyo itaangazia pia sababu za ufaulu hafifu wa somo hilo la EDK katika shule mablimbali hapa nchini.

Athari za elimu ya Kisekyula
Kwa upande mwingine, Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Sunna Tanzania (BASUTA), Sheikh Muhammad Issa akitoa mada yenye anuani ya ‘Umuhimu wa Mfumo wa Elimu wa Kiislamu katika Ulimwengu’ kwenye semina hiyo, alisema kuwa maadui wa Uislamu walitengeneza mfumo wa elimu ya kisekyula ambao umejengeka katika msingi wa kuwafuga wanafunzi wa Kiislamu na siyo kuwalea kimaadili.

“Mfumo wa elimu ya kisekyula uliopo duniani uliwekwa kimkakati ili kuwafuga wanafunzi kwa kugawa elimu katika nyanja kuu tatu ambazo ni maarifa ya sayansi ya asili (natural science), sayansi ya jamii (social science) na masuala jamii (humanities) na kutotilia manani suala la maadili,” alisema.

Aidha, Sheikh Issa alisema ili kukabiliana na athari hizo hasi za mfumo wa elimu ya kisekyula, walimu wa Kiislamu hawana budi kueneza elimu ya Kiislamu kama njia mbadala.

“Mfumo hauwezi kuondolewa isipokuwa na mfumo mwingine. Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) alipokuja na Uislamu kama mfumo wa maisha, mifumo yote ya binadamu ilishindwa kupambana na Uislamu hivyo waalimu hawana budi kutumia Uislamu kupambana na athari hasi za elimu ya kisekyula,” Sheikh Issa amesema.

Semina hiyo ilifunguliwa na Sheikh Alhadi Mussa, Sheikh wa mkoa wa Dar es Salaam. Miongoni mwa masheikh wengine wakubwa waliohudhuria semina hiyo ni Sheikh Mussa Kundecha, Amir wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu na masheikh wengine.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close