-Matukio

Hongereni wote mliojitokeza Misk ya Roho

Oktoba 28 ya mwaka huu ilikuwa ni siku nzuri ya Waislamu hapa nchini kujumuika kwa minajili ya kupata ujumbe wa dini yao tukufu ya Uislamu. Mjumuiko huo ulifanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam ambapo Waislamu walijazwa maarifa yaliyomo ndani ya dini yao tukufu ya Uislamu kutoka kwa mtoa mada mmoja hadi mwingine hadi watoa mada wote wanane walipomaliza mada zao.

Na ukweli wa mambo si waliohudhuria tu ndio walishehenezwa na maarifa hayo bali hata waliokuwa nyumbani, njiani na kwengineko waliweza kupata pia ujumbe huo kwa kuwa baadhi ya vituo vya runinga, redio na mitandao ya kijamii kama Facebook na Youtube vilirushwa tukio hilo mubashara.

Ni faraja sana kuona tukio la kidini likihudhuriwa na umati mkubwa kama ule ndani ya ukumbi wa Diamond Jubilee na mamilioni wengine wakifuatilia kupitia vyombo vya habari. Hii ni ishara mojawapo kuwa dini ya kweli ya Mwenyezi Mungu inawafuasi wa kutosha na wenye mahaba na Mola wao kama kaulimbiu ya kongamano hilo ilivyoyosomeka “Utukufu wake”.

Waislamu hao walipata ujumbe maridhawa wa Kiislamu kutoka kwa wahadhiri wa ndani na nje ya nchi yetu ambao ni pamoja na Sheikh Yusuf Abdi na Sheikh Jamaldin Osman kutoka Kenya, Sheikh Zuberi Bizimana (Burundi), Sheikh Ally Kajura (Rwanda) na Sheikh Muhammad Abduweli kutoka Uganda. Na kwa hapa nchini walikuwemo kina Sheikh Dourmohamed Issa, Sheikh Ally Jumanne na Sheikh Abdulrahman Mhina (Baba Kiruwasha)..

Wahadhiri hao waligusia masuala mbalimbali yakiwemo ya utukufu wa Mwenyezi Mungu, mahusiano ya mja na Mola wake, Muislamu na toba, Muislamu katika ndoa kama moja ya dalili za Allah. Masuala haya yameelezwa kwa kina katika habari zilizochapwa katika toleo la gazeti iman.

 

Kimsingi hayo yote ni masuala muhimu sana kwa Muislamu kuyafahamu kwani yanamjenga kiimani na kumtanabaisha juu ya matendo sahihi ya Uislamu na vipi aishi kulingana na matendo hayo.
Hivyo tunasema Waislamu walipata elimu kubwa wanayotakiwa kuifanyia kazi ipasavyo kwa ajili ya faida yao ya  hapa duniani na akhera.

Tuseme tu tuna kila sababu ya kuwashukuru na kuwapongeza wahadhiri hao kwani walifanya kazi kubwa ya kukonga nyoyo za wahudhuriaji. Si kazi rahisi sana kuwafanya watu wake kwa zaidi ya saa 10 wakiwa na bashasha, na hamu ya kusilikiza muda wote, kama tunavyofahamu akili ya binadamu yoyote huchoka, ila kwenye kongamano hilo wengi walionesha kutochoka.

Pia hatuna budi kuwapongeza watu wote waliohudhuria Kongamano hilo na wale waliyokuwa wakifuatilia kutoka sehemu mbalimbali. Kuhudhuria kwao ndio ilikuwa chachu ya kufanikiwa kwa kongamano hilo na tunazidi kuwaomba waendelee kushiriki katika makongamano mengine.

Aidha tunawapongeza na kuwashukuru wadhamini wote wa Kongamano kwa msaada wao mkubwa ambao umewezesha kung’ara kwa kongamano
hilo. Wadhamini hao ni wale wa Platinum ambao ni Asas Dairies Ltd ya Iringa, Afya pure drinking water na Azam TV. Kwa upande wa dha- habu (Gold) ni Usangu logistics(T) Limited, Dar fresh Milk, O-GAS na Fedha (Silver) ni kampuni ya Mafuta ya ATN. Na shaba (Bronze sponsors) ni MOROBEST, Simba Oil, Cam Gas, Dar center na Carmel floor milk.

Tunasema kazi waliyoifanya wadhamini hao ni kubwa sana ambayo mwenye uwezo wa kuwalipa malipo yaliyobora ni Mwenyewe Mwenyezi Mungu.

Mwisho lakini si kwa umuhimu tunaupongeza uongozi wa Taasisi ya The Islamic Foundation(TIF) kwa kuandaa kongamano hilo lenye tija kubwa kwa Waislamu. Tunazidi kuwasihi waendelee kuandaa makongamano hayo kwa ajili ya kuendeleza dini ya Uislamu na tunaimani Uislamu utazidi kushamiri InshaAllah!

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close