-

FALSAFA YA SADAKA

Ulichotoa Kimebakia,ulichotumia kimemalizika

Aisha (Allah amridhie) amesimulia kwamba walichinja mbuzi. Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) Akasema: “Kuna kilichobaki?” Akasema: “Hakuna kilichobakia isipokuwa bega lake.” Akasema (Mtume): “Mbuzi wote amebaki isipokuwa bega lake” (Tirmidhy, na al-Baaniy Amesema ni sahihi).

Katika tukio hili tunajifunza umuhimu wa kujitolea na thamani ya kile alichokitoa mtu. Kwa kawaida, nafsi huona kama inapungukiwa pale mtu anapotoa sadaka. Mwingine hulimbikiza na mwingine hufanya ubakhili kwa kutumia mwenyewe.

Lakini katika tukio hili, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) anageuza mitazamo ya watu na kuwafanya wawe na fikra chanya katika suala zima la kutoa sadaka, yaani waamini kuwa kile walichotoa ndicho kilichobakia na walichotumia wao ndicho kilichomalizika. Katika tukio hili, mbuzi alichinjwa nyumbani kwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) ikawa sehemu kubwa ya mbuzi yule imetolewa sadaka kwa watu. Mtume alipokuja kuulizia kilichobakia, mkewe Aisha (Allah amridhie) alimwambia: “Hakuna kilichobaki isipokuwa bega tu.”

Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) akamwambia kuwa, kile walichokitoa sadaka ndicho kilichobaki na kile kilichobakishwa pale ndicho kilichokwisha. Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) anatufundisha kuwa sadaka anayoitoa mtu ndiyo sehemu anayoibakisha katika mali yake.

Kutoka kwa Abdullah bin Shikhiiri (Allah amridhie) amesema: “Nilimjia Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) Nikamkuta akisoma, ‘Al-haakumut Takaathur’ (Kumekushughulisheni kutafuta wingi (mali), Mpaka mje makaburini!). Akasema (Mtume), ‘Binadamu anasema mali yangu, mali yangu. Hivi una mali isipokuwa ile uliyokula ukaimaliza, au uliyoivaa ukaichakaza au uliyoitoa sadaka ukaibakisha,” (Muslim).

Haya ni maneno mengine ya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) akituonesha fikra ya mwanadamu juu ya mali ilivyokuwa kinyume na uhalisia. Anatufahamisha kuwa mwanadamu hutoa madai kuwa hii ni mali yangu mali yangu, hata hivyo, ukweli ni kuwa hana chake isipokuwa kile ambacho ameshakula akakimaliza, au alichotumia katika mavazi akayachakaza au kile alichokitoa sadaka kikawa amekibakisha.

Zaidi ya vitu hivyo, mwanadamu hana chochote kwani akiondoka wakati wowote kile alichokuwa akililia kuwa ni chake kinageuka kuwa cha warithi wake.

Mafundisho haya ya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) yanavyotujenga katika kuamini kuwa mahali pakuwekeza mali ni kutoa sadaka. Huu ndiyo uwekezaji mzuri kwani kile anachotoa anajiwekea akiba atakayoikuta mbele ya Allah Aliyetukuka.

Allah anasema: “Na mkopesheni Mwenyezi Mungu mkopo mwema. Na kheri yoyote mnayoitanguliza kwa ajili ya nafsi zenu mtaikuta kwa Mwenyezi Mungu, imekuwa bora zaidi, na ina thawabu kubwa sana. Na mtakeni msamaha Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu,” (Qur’an, 73:20).

Katika suala zima la kujitolea, Allah anawatoa hofu waja wake na kuwathibitishia kuwa wanapotoa, Yeye huwapa mbadala. Hivyo basi, njia bora ya kuchuma ziada ya kile ulichonacho ni kujitolea katika njia za kheri kile kinachozidi mahitaji yako ili Allah aendelee kukufanyia wepesi katika njia za chumo lako kwa kukupa mbadala wa kile unachokitoa.

Allah anasema: ”Sema, ‘Kwa hakika Mola wangu Mlezi humkunjulia riziki na humdhikisha amtakaye katika waja wake. Na chochote mtakachokitoa Yeye atakilipa. Naye ni Mbora wa wanao ruzuku.’” (Qur’an, 34:39).

Katika Aya nyingine, Allah anauliza: “Ni nani atakayemkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mwema, ili amrudishie maradufu, na apate malipo ya ukarimu,” (Qur’an, 57:11). Mkopo unaokusudiwa hapa ni kujitolea katika kheri mbalimbali kwa ajili ya kutaka radhi za Allah. Allah Aliyetukuka anatufahamisha kuwa, sisi wanadamu ni wasimamizi tu katika vile alivyotupatia na hatuna umiliki wa hakika, bali mmiliki wa vyote ni yeye Allah Aliyetukuka.

Mwenyezi Mungu anatutaka tujitolee katika hivyo ambavyo ametupa dhamana ya usimamizi. “Muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake; na toeni katika alivyokufanyeni nyinyi kuwa ni waangalizi wake. Basi walioamini miongoni mwenu, na wakatoa, wana malipo makubwa,” (Qur’an, 57:7).

Tutoe katika hivi ambavyo Allah ametufanya kuwa ni waangalizi tu, na si wamiliki kwani ufalme wa mbingu na ardhi ni wa Allah Aliyetukuka.

Ukitaka kupata kheri nyingi, faidika na dua ya Malaika hawa ambao kila siku wanamuomba Allah ampe mtoaji mbadala wa kile alichotoa na kumuombea bakhili uharibifu. Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Hakuna siku ambayo hupambazukiwa waja isipokuwa na Malaika wawili huteremka, mmoja wao husema, ‘Ewe Mola mpe badala mwenye kutoa’ na mwingine husema, ‘Mpe uharibifu mwenye kuzuia’” (Bukhari na Muslim). Allah anatuuliza swali la kutuzindua juu ya uzito tulionao katika kujitolea: “Na mna nini hata hamtoi katika Njia ya Mwenyezi Allah, na hali urithi wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu?” (Qur’an, 57:10).

Tuhakikishe tunahifadhi na kuwekeza kile alichotupa Allah Aliyetukuka kwa kukitoa katika njia zake ili tukayakute matunda yake mbele ya Allah Aliyetukuka.

Tukio hili linatufundisha tabia walizokuwa nazo wema waliopita, linawapa msukumo wanawake wawe ni wenye kujitolea kama alivyofanya mama Aisha (Allah amridhie), pia linawakumbusha wanaume kuridhika na kilichobakia katika kile ambacho amekitoa mkewe kumpa mwenye shida.

Tags
Show More

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button
Close
Close