-1. Habari1. TIF News

DC Wilaya ya Mwanga Aimwagia Sifa TIF

NA AMIRI MVUNGI, ARUSHA

Mkuu wa Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, Aroon Mbogho (kulia) akiteta jambo na Mwenyekiti wa The Islamic Foundation, Aref Nahdi.

Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro Aroon Mbogho amemshukuru Mwenyekiti wa Taasisi ya The Islamic Foundation (TIF), Aref Nahdi kwa juhudi zake za kusaidia kwake huduma muhimu za kijamii kwa wakazi wa kijiji cha Masumbeni kilichopo tarafa ya Ugweno. Mbogho ametoa shukrani hizo wakati Mwenyekiti huyo wa TIF alipomtembela ofisini kwake na kueleza kuwa, serikali haiwezi kufanya kila jambo bila kushirikiana na wadau wa maendeleo hivyo anaishukuru TIF kwa kuahidi misaada hiyo ambayo kwa hakika itasaidia kubadilisha taswira ya maendeleo katika wilaya hiyo. “Sijawahi kutembelewa na ugeni ambao unazungumzia masuala ya mafanikio na maendeleo ya wananchi, hivyo taasisi ya The Islamic Foundation imeonesha mwanga wa kubadilisha wilaya hii,” alisema Mkuu huyo wa wilaya. Awali, Mwenyekiti wa TIF, Aref Nahdi alisema taasisi yake inatarajia kutoa misada ya uchimbaji wa visima vya maji, ukarabati wa ofisi ya kata, ujenzi wa zahanati na vyerehani zaidi ya kumi kwa akina mama. Mwenyekiti Nahdi aahidi misaada Mwenyekiti aliwaambia wakazi wa kijiji cha Masumbeni: “Mimi furaha yangu kubwa ni kuona mna raha na dini yenu na mnaonyesha ushirikiano wa karibu katika mambo ya msingi ya kuipeleka dini ya Mwenyezi Mungu mbele,” alisema Nahdi. Mwenyekiti Nahdi alipata fursa ya kuzungumza na waumini wa dini ya Kiislamu wa kijiji hicho na baadaye kuzuru eneo unapojengwa msikiti wa kijiji ambapo aliahidi kutoa Shilingi Milioni tatu ili kuharakisha mchakato wa ujenzi huo. Naye Mkurugenzi wa usimamizi wa miradi ya TIF kanda ya kaskazini Ramadhani Mfinanga ambaye aliambatana na Mwenyekiti Nahdi alisema, kwa sasa taasisi imejikita katika kupeleka huduma muhimu za kijamii katika maeneo ya vijijini ambayo kwa kiasi kikubwa yanakabiliwa na changamoto za ukosefu wa misikiti na huduma ya maji. Mbali na misaada hiyo, TIF kwa kushirikiana na taasisi ya Islamic Development Foundation (IDF) inatarajia kujenga chuo cha elimu ya sayansi ambacho kinatarajiwa kuwa mkombozi mkubwa kwa vijana wa Kiislamu. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa IDF, Amal Temu ameishukuru serikali kutokana na uamuzi wake wa kurejesha eneo la ardhi na kuwa chini ya Waislamu, kwani lengo ni kujengwa chuo cha elimu ya sayansi kitakachotoa ufumbuzi wa kuzalisha vijana waliobobea kwenye masomo ya sayansi. Amal alisema hatua ya Mwenyekiti wa TIF kufika wilayani Mwanga kwa lengo la kujionea eneo hilo na kuahidi kutoa gharama zote za upimaji wa eneo hilo ni ishara tosha kwamba ujenzi wa chuo utaanza mara moja ili kufikia malengo yaliyokusudiwa. “Ziara aliyoifanya Mwenyekiti wilayani Mwanga ni ya kipekee na yenye manufaa makubwa kwa wananchi kwani amethibitisha ni kwa jinsi gani alivyo na upendo, huruma na asiyebagua watu wa madhehebu mengine,” alisema Amali.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close