-

Bima ya Kiislamu yanukia nchini

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima nchini (TIRA) imesema inapitia maombi ya kampuni tatu zilizoomba kutoa huduma za bima ya Kiislamu (Takaful). Akinukuliwa gazeti la The Citizen la Machi 25 mwaka huu, Kamishna Mkuu wa TIRA, Dkt. Baghayo Saqware ametaja kampuni zilizoomba kutoa huduma hiyo kuwa ni Azam, Mo Insurance na Kampuni moja ya Zanzibar, ambazo zote zinamilikiwa na Watanzania.

Dkt. Saqware amesema kwa sasa wanapitia maombi hayo ili kuona kama kampuni hizo zimekidhi vigezo na kuongeza kuwa vigezo hivyo ni sawa na vinavyofuatwa na kampuni zingine.

“Vigezo vya kusajili kampuni zitakazotoa huduma hiyo ya takaful ni sawa na vigezo vinavyozingatiwa na kampuni nyingine, ikiwemo mitaji, isipokuwa tu msisitizo utahusu Sheria za Kiislamu,” alisema Dkt. Saqware.

Pia, Kamishna huyo alibainisha ongezeko la uhitaji wa huduma hiyo na kutoa wito kwa kampuni zingine kuangalia jinsi ya kutoa huduma za aina hiyo ili kupanua wigo. Taarifa hiyo inayotoa matumaini inakuja takribani mitano tangu kuanza kwa mchakato wa uundwaji wa kanuni za kusimamia bima za Kiislamu. Ni mwaka 2015 ambapo gazeti la The Citizen, lilinakili taarifa ya aliyekuwa Kamishna Mkuu wa TIRA, Israel Kamuzora, akisema kuwa mchakato wa uundwaji wa kanuni hizo ulikuwa katika hatua za mwisho. “Sasa tupo hatua ya mwisho ambapo tunatafuta maoni ya wadau na tunatumai kanuni zitakuwa tayari kabla ya mwisho wa mwaka,” Kamuzora alinukuliwa.

Furaha ya Waislamu
Taarifa ya Dkt. Saqware kuhusu kampuni tatu zilizoomba kutoa huduma hiyo inarejesha matumaini ya Waislamu wanaohitaji Takaful kwa miaka mingi. Baadhi ya Waislamu wametaja hatua hii kuwa ni ishara njema kwani itawapa fursa ya kuingia kwenye huduma ambayo haina haramu ndani yake. Mmoja wa Waislamu, Rahim Juma wa Tanga amesema bima zingine zinafungamana na riba na pia zinakiuka kanuni za miamala ya Kiislamu hivyo imekuwa ngumu kwa Waislamu kuingia huko.

“Tunafurahi kusikia kampuni hizo zimejitokeza kutoa huduma za takaful. Hiyo itatuondolea kikwazo sisi Waislamu tunaokwepa miamala ya haramu kama Uislamu unavyotaka,” alisema Juma.

Naye Shadya Ramadhani wa Kibaha alipongeza hatua hiyo na kusema kuwa itafungua fursa kwa Waislamu siyo tu kupata bima ya halali lakini pia kwa kampuni za Waislamu kuingia katika sekta hiyo na hivyo kushiriki katika kukuza uchumi hapa nchini. Kwa upande wake, Sheikh Muhammad Issa ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Sunna nchini (Basuta) amesema: “Takaful inahitajika sana ili kufanya huduma za kibenki za Kiislamu ziwe vile zinavyotakiwa. Bila ya uwepo wa Takaful, mtu anakopa Kiislamu lakini ananunua bima yenye haramu, tatizo ambalo sasa litaondoka kwa ujio wa Takaful,” alisema Sheikh Muhammad.

Utafiti wa Takaful
TIRA ilifanya utafiti mwaka 2012 juu ya Takaful na kutoa mapendekezo serikalini ya kuanzishwa kwake. Lakini pia TIRA ilipendekeza zitungwe kanuni za kuruhusu aina hiyo ya bima. Kwa mujibu wa ripoti ya Ernest & Young inaonesha kuwa kwa mwaka 2018, soko la Takaful duniani lilikadiriwa kuwa na thamani ya dola bilioni 1 Hiyo ni ishara njema kuwa Takaful inazidi kupata wateja wengi na hivyo kuwa na wigo mpana katika masoko duniani. Katika bara la Afrika, tayari nchi kadhaa zikiwemo Morocco, Afrika Kusini, Kenya tayari zina huduma za bima ya Kiislamu.

Kwa nini Takaful?
Kuna tofauti kadhaa katika utoaji wa huduma za bima ya Kiislamu ukilinganisha na bima za kawaida. Katika bima ya Kiislamu, mwanachama ana haki ya kupata gawio kwa kiasi ambacho kinabaki kutokana na fedha zilizokusanywa kwa mwaka, jambo ambalo halipo katika bima za kawaida. Hali kadhalika, mwanachama asipopata janga au ajali, fedha zake zinakuwa bado zipo isipokuwa kwa kile kitakachopungua kwa kuchagia kulipia bima za wenzake waliopata ajali.

Katika Takaful, wanaoingia humo ndiyo wamiliki wa mfuko wa bima tofauti na bima za kawaida ambazo wamiliki ni wenye kampuni ya bima. Bima ya Kiislamu hairuhusu mtu mmoja au taasisi kunufaika peke yake. Wanachama wanaochangia katika mfuko ndiyo wanufaika wakubwa. Katika bima ya Kiislamu, mwanachama akipata tatizo atalipwa kulingana na tatizo lake, lakini mwisho wa mwaka waendeshaji watapiga mahesabu na kama kuna kiasi ambacho kimebaki basi kitagawiwa kwa wanachama.

Kuhusu suala la uendeshaji, taasisi ya bima ya Kiislamu itaendeshwa zaidi kupitia ada zitakazolipwa na wanachama wake na pia gawio la uwekezaji halali wa fedha za bima ambao faida yake wenye mfuko wa bima na kampuni ya bima hugawana.

Faida nyingine ya bima ya Kiislamu ni kuepusha watu dhidi ya riba. Inajulikana wazi kuwa, Uislamu unakataza kujihusisha na shughuli za kiuchumi zenye riba ndani yake, lakini Tanzania kwa sasa hakuna mbadala wa taasisi ya bima isiyojihusisha na riba. Kwa sababu hiyo, wakati kuendesha chombo cha usafiri bila bima ni makosa, kwa hali ya sasa Muislamu ambaye dini inamkataza riba hana namna zaidi ya kuingia katika dimbwi la riba kwa kulazimika kukata bima za kawaida.

Malengo ya bima
Malengo makuu ya uwepo wa bima ya aina yeyote ni kumnusuru yule aliyekata bima asipate hasara na kuyumba pindi anapopata matatizo ama majanga yasiyotarajiwa kumtokea. Majanga hayo yanaweza kuwa kama ajali, moto, kimbunga, mafuriko, ukame na kadhalika. Aidha, bima ni kinga muhimu inayomuacha mwenye kukata akiwa na amani ya moyo kwa kuweza kuwa huru kufanya shughuli zake bila kuhofia majanga yanayoweza kutokea mbele.

Baadhi ya wataalamu wameita bima, akiba isiyooza ambayo itatumika katika kipindi ambacho unahitaji msaada wa haraka wa kukuvusha kutoka sehemu moja kwenda nyingine baada ya mkwamo usiotarajiwa katika maisha yako ya kila siku.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close