-

Balozi Kilima Ahimiza Tabia Njema, Ataka Wazazi Wasiwachagulie Watoto Masomo

Balozi wa Tanzania nchini Oman Abdallah Kilima amewataka vijana kuwa mabalozi wa Uislamu kwa kudhihirisha tabia njema mbele ya jamii ili kuijengea sifa na heshima dini tukufu ya Uislamu. Balozi Kilima alitoa wito huo wakati wa hafla ya kuwapongeza na kuwazawadia wanafunzi waliofanya vizuri kwenye mtihani wa kidato cha nne mwaka 2016 iliyofanyika kwenye hoteli ya Lamada Manispaa ya Ilala jijini Dar es salaam.

Kilima alisema vijana ndiyo nguzo ya umma wa Kiislamu hivyo ni vema wakaonesha mfano wa tabia njema kwenye jamii inayowazunguka. “Popote mnapokuwa mnapaswa kudhihirisha Uislamu wenu kwa kufanya matendo mema ili kuijengea heshima dini yenu, lakini pia jiepusheni na maovu kwani kufanya hivyo kutapelekea fedheha na aibu kwa Waislamu na Uislamu,” alidokeza Balozi Kilima.

Aidha, Kilima aliwakumbusha wahitimu hao kutambua lengo la kuwepo kwao duniani ambalo ni kumuabudu Mwenyezi Mungu, huku akiwasisitiza kusoma kwa bidii na unyenyekevu kwa kuwa jambo la kutafuta elimu ni ibada kama zilivyo ibada nyingine. Balozi Kilima aliongeza kusema, kupata cheti (Certificate), Stashahada (Diploma) au Shahada (Degree) siyo ngazi ya kupatia ajira kama ambavyo wengi hudhani.

Elimu ni ngazi ya kumfikisha mtu kwenye maisha bora, na nyinyi kama vijana mnatakiwa muitafsiri elimu katika vitendo ili muweze kujiajiri kwani elimu ni nyenzo ya kumuwezesha mtu kuyaendea maisha yake kwa ustadi na uelewa zaidi,” alibainisha.

Akitoa nasaha zake katika hafla hiyo, Mkuu wa Chuo cha Uhandisi na Teknolojia cha jijini Dar es Salaam (AMCET) Dkt. Ibrahim Hamduni, aliwashauri wanafunzi wanaotarajia kujiunga na kidatio cha nne mwaka huu kusimamia malengo yao, na huku wakimtegemea Mwenyezi Mungu katika masomo yao.

Hili ndilo jambo kubwa kwenye mafanikio ya elimu hivyo ni wajibu kumuomba Mwenyezi Mungu na kumtegemea ili awaongezee ufahamu na kuwafanyia wapesi kwenye masomo yenu” alisisitiza Dkt. Hamduni.

Katika hatua nyingine, Dkt. Hamduni alitoa wito kwa wazazi kuacha kasumba ya kuwachagulia watoto wao masomo (subjects combination) wasiyoyapenda, na ambayo hawana uweledi nayo wakati wanapojiunga na elimu ya kidato cha tano na sita kwani kufanya hivyo ni kuwapotezea malengo ya baadaye.

Hamduni alisema wanafunzi wengi husoma kwa bidii lakini mwishowe wanavuna kile wasichokitaraji kwa sababu ya kushawishiwa kusomea fani wasizozipenda. Naye aliyekuwa mgeni rasmi, katika hafla hiyo Dkt Abdulqadir Nasser Aljahdhamiy kutoka nchini Oman amewashauri wahitimu kutumia elimu waliyoipata kubuni ajira binafsi, huku akiwaonya baadhi ya wanafunzi ambao hutamani kupata mafanikio ya haraka pasipo kuwajibika.

Mwanafunzi anatakiwa ajue malengo, thamani yake na ajitambue. Tatizo ni kwamba, wanafunzi wanasoma ili wawe watu fulani badala ya kuinufaisha jamii,” alisema Dkt Abdulqadir.

Dkt. Abdulqadir alisema wazazi wana sehemu kubwa ya malezi ya wanafunzi na kutambua vipaji vya watoto wao kutokana na ukaribu uliopo baina yao kabla ya kuwapeleka shule. Akilinganisha mfumo wa elimu uliopo sasa na ule wa zamani Dkt. Abdulqadir alibainisha kuwa, mfumo wa elimu ya Tanzania kwa miaka ya zamani unatofautiana kwa kiasi kikubwa na wa sasa. Alisema asilimia kubwa ya mawaziri na wahadhiri wa vyuo vikuu vya nchini Oman walizaliwa na kusomea Tanzania.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close