-

12 wahitimu Qiraa mbili za Qur’an Dar

Wanafunzi 12 kutoka kituo cha Al-Hikma Foundation cha kuhifadhisha Qur’an cha jijini Dar es Salaam wametunukiwa vyeti (Ijaaza) baada ya kuhitimu Qiraa mbili za Qur’an, Qiraa ya Hafswi kutoka kwa ‘Aswim na riwaya zake mbili za Shaatwibiyyah na Shughbah.

Mwalimu aliyewasomesha wanafunzi hao visomo hivyo vya Quran ni AbdulMannaan Mohammad Hassan ambaye amehitimu aina 10 za visomo vya Qur’an kwa upokezi/mlolongo (sanad) unaokwenda hadi kwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie).

Mwalimu huyo, AbdulMannaan, ambaye daraja ya sanad yake ni ya 29 mpaka kufika kwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie), ndiye aliyewapa vijana hao Ijaaza (Ithbati) ya kuhitimu aina hizo mbili za visomo vya Qur’an.

Mwalimu AbdulMannaan ana historia ya kuvutia. Alihifadhi Qur’an nyumbani akiwa na umri wa miaka tisa. Kisha akahudhuria madrasa kadhaa ndogo ndogo nchini Tanzania na Kenya katika miji ya Nairobi- Mombasa. Akiwa na umri wa miaka 12 tu, alikwenda Mauritania ambako alikaa huko miaka minne akisoma zaidi mambo ya dini.

Baada ya kumaliza miaka yake minne huko Mauritania, alikwenda Misri katika mji wa Alexandria katika chuo cha Mahdil Furqaan, ambako alisoma kwa mwaka mmoja. Akiwa huko huko alipokutana na mwalimu wake aliyemsomesha Qiraa 10 za Qur’an ambaye ni mmoja wa masheikh wakubwa nchini Misri, aitwaye Dkt. Ahmad Hamiid.

Baada ya kuhitimu Qiraa hizo 10 kwa miaka miwili, Sheikh Dkt. Hamiid alimpa ijaaza AbdulManaan, ijaza ambayo, kama tulivyotaja ina mlolongo wa watu 29 kabla ya kufika kwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie).

Katika hafla ya kuwatunuku vijana hao vyeti iliyofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency Kilimanjaro, mwalimu huyo alitaja sanad yake, mlolongo wa Masheikh waliomfundisha – jina moja baada ya jingine – mpaka kufikia kwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie).

Vijana hao ambao waliohitimu ni miongoni mwa walimu 35 kutoka Al-Hikma Foundation, na wamefikia hatua hiyo baada ya kupitia mafunzo ya mwaka mmoja na hivyo kujiongezea maarifa katika ufundishaji wao wa Qur’an.

Akiongea katika hafla hiyo, mgeni rasmi, Mufti wa Tanzania, Abubakar Zubeir aliwapongeza vijana hao na kuwataka watumie elimu waliyoipata ili kuzalisha wasomi wengi zaidi. “Niwapongeze vijana hawa na niseme jambo hili la leo ni zuri, nani imani yangu kuwa wahitimu hawa watasaidia kuzalisha wasomi wengi zaidi wa Qur’an,” alisema Mufti. Mufti Zubeir alisema, alipokuja Mfalme wa Morocco na kutoa zawadi ya misahafu iliyoandikwa kwa Qiraa ya Warshy, Waislamu wasiojua aina za visomo vya Qur’an walishangaa.

Aidha, Mufti Zubeir alisema Uislamu siyo dini ya ugomvi kama inavyodhaniwa na baadhi ya watu. “Uislamu sio ugomvi, Uislamu siyo fujo, Uislamu siyo tabia za hovyo hovyo, Uislamu ni dini ya upendo,” alisema Mufti Zubeir.

Naye Rais wa kituo hicho cha Al-Hikma Foundation, Sheikh Abdul-qadir Al-Ahdaly, akiongea katika hafla hiyo, alisema kwamba, vijana waliohitimu kielelezo cha ubora wa mafundisho ya Qur’an, na kisha akawahimiza wajipambe na maadili mema.

Mufti Abubakar Zubeir aliwapongeza vijana hao na kuwataka watumie elimu waliyoipata ili kuzalisha wasomi wengi zaidi.

Sheikh Abdulqadir alisema yote hayo yasingewezekana kama siyo kuwa na amani na utulivu wa nchi yetu. “Serikali yetu imeruhusu uhuru wa kuabudu na Uislamu ni dini ya amani ndiyo maana tunaweza kufanya yote haya,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Al-Hikma Foundation, Sheikh Nurdin Kishki amesema kituo chake hicho kitaendelea kuwajenga walimu ili kuijenga jamii bora. “Tukimjenga Mwalimu ndiyo pia tunaijenga jamii nzima na kwa namna bora. Hivyo, mafunzo haya ya Qiraa cha Qur’an yataendelea kutolewa,” alisema Sheikh Kishki. Pia Sheikh Kishki alisema, hafla hiyo ni maandalizi ya mashindano ya usomaji Qur’an ya Afrika Mashariki yatakayofanyika Mei 19 mwaka huu katika Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam.

Wahitimu
Nao baadhi ya wahitimu hao wamesema mafunzo hayo yamezidi kuwafanya kuwa bora katika kuielewa Qur’an. “Nimefarijika sana kupata hii ijaaza kwani imeniongezea maarifa katika kuifahamu Qur’an,” alisema Nasruddin Hashim Chilanga. Mhitimu mwingine, Mussa Abdallah Salum alisema: “Ni muhimu sana kupanua wigo wa elimu, hivyo niwashauri walimu wenzangu wa Qur’an wajitahidi kusoma Qiraa mbalimbali.”

Wahitimu waliotunukiwa vyeti ni Rajab Juma Ngota, Abdilah Zuberi Hamad, Mohammed Faiz Lardhi, Sharifu Swaleh Masudi na Nasruddin Hashim Chilanga. Wengine ni Burhan Abdallah Shirazi, Abdallah Khamis Limbumba, Mussa Abdallah Salum, Ismail Muhamed Didas, Seif Ramadhan Zombe na Ahmad Hamisi Mrisho.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close