1. Habari1. TIF News

Mwenyekiti TIF aahidi makongamano mengine makubwa zaidi

Aref Nahdi, Mwenyekiti wa The Islamic Foundation (TIF) amesema kuwa taasisi yake inatarajia kuja na makongamano makubwa zaidi kwa ajili ya kutoa da’awa kwa Waislamu hapa nchini.

Mwenyekiti Aref Nahdi aliyasema hayo kwenye kongamano la Misk ya Roho lililofanyika Jumapili iliyopita jijini Dar es Salaam ambapo alisema Waislamu wengi wameonesha hamasa kwenye kongamano la Misk ya roho na mengine, hivyo inabidi wapatiwe lingine kubwa zaidi.

Nahdi alisema kuwa kongamano la Misk ya Roho limefanikiwa kwa kiasi kikubwa na limekidhi matarajio ya Waislamu wengi. Alisema:

“Tunamshukuru Allah, kongamano lilikuwa zuri, watu wengi wamelifurahia, wameelimika  na hicho ndicho tulichokitaka zaidi,”

Pia Nahdi aliwashukuru watu wote waliofika kwenye kongamano hilo na kusema kufika kwao ndiyo  mafanikio ya kongamano.

“Napenda kushukuru wageni wetu, Masheikh wetu  na Munshid waliokubali mualiko wetu na kuja na hivyo kulifanya hili kongamano kuwa la mafanikio….Vile  vile bila kusahau vijana wetu wa volunteers (wakujitolea) kuweza kufanikisha hili kongamano katika utendaji wao mzuri kama tunavyona mambo yalivyopendeza…..Na Misk ya Roho tunategemea kuwa ni brand yetu ya mihadhara ambayo tutaifanya kila mwaka,”

Naye Mkurugenzi wa Vyombo vya Habari vya Imaan vilivyoko chini ya TIF, Ahmed Bawazir amewaomba Waislamu wazidi kuvichangia vyombo hivyo ili viendelee kutoa elimu na habari kwa Waislamu.

“Ndugu zangu hivi vyombo tunavyoviendesha havitengenezi faida, ni vyombo vya kutoa da’awa, hivyo tunaomba mzidi kuvichangia,”

Pia Bawazir alitoa wito kwa Waislamu kupeleka matangazo ya biashara kwenye vyombo hivyo ili kusaidia kuviendesha. Vyombo vya habari vya Imaan ni pamoja na Redio Imaan, TV Imaan na gazeti Imaan. Kufanyika kwa kongamano la Misk ya Roho hapa nchini ni muendelezo wa juhudi za Taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) za kuwaleta Msheikh na Wanazuoni kutoka mataifa mbalimbali ulimwenguni kwa ajili ya kufanya da’awa.

Mwaka 2015 TIF yenye makao yake makuu mkoani Morogoro ilifanikiwa kumleta Mhubiri wa Kimataifa kutoka nchini Zimbabwe, Sheikh Ismail bin Musa Menk maarufu Mufti Menk, na mwaka 2016 ilimleta Mhubiri wa kimataifa na Mkuu wa Kituo cha Kiislamu cha Australia Markaz Islaami, Ustadh Wahaj Tarin.

Wakati huo huo Mwenyekiti Nahdi aliwashukuru wadhamini wote waliojitokeza kufadhili kongamano hilo na kuwaomba wazidi kuunga mkono shughuli za TIF.

Tags
Show More

Related Articles

Close
Close