
Saikolojia: Matarajio yasiyofikiwa yanavyotuathiri kimaisha
Aghlab, tunakuwa na matarajio mengi katika maisha lakini ni muhimu sana kudhibiti matarajio yetu kwa sababu mara nyingi yasipofikiwa huzalisha maumivu na hali ya kuvunjika moyo.
Matarajio ni kitu tata. Kwa upande mmoja, hutuhamasisha na kuzielekeza tabia zetu kuelekea malengo na mafanikio. Kwa upande mwingine, matarajio, hasa pale yasipofikiwa, yanasababisha hali ya kukatishwa tamaa, hali ya tashwishi, wasiwasi, na hata uchovu.
Hivyo basi, matarajio huathiri tabia yetu kwa namna nyingi, hasa yasipofikiwa. Na ukweli ni kuwa matarajio mengi hayafikiwi, kwa mujibu wa takwimu. Angalia mifano hii.
Kila mtu anataka kuwa mkurugenzi mtendaji lakini ni mtu mmoja tu anayeweza kushikilia cheo hicho katika kampuni yoyote. Matarajio ya ndoa ya kudumu na yenye furaha ni jambo la kawaida, lakini viwango vya talaka bado viko juu. Licha ya kuwa na matarajio makubwa, biashara za hadi asilimia 90 ya wajasiriamali hushindwa. Si hivyo tu, wengi tuna malengo ya kuwa mamilionea lakini hatuyafikii.
Matarajio yanakujaje? Matarajio huja kama matokeo ya malengo tunayojiwekea sisi wenyewe na ambayo hatimaye yanatuweka katika mazingira yaliyojaa shinikizo.
Kulingana na utafiti uliochapishwa katika Jarida la Personality and Social Psychology (2017), watu waliojiwekea matarajio ya juu wanakabiliwa na shida za wasiwasi na uchovu.
Shida nyingine inayotokana na matarajio makubwa hujitokeza katika uhusiano. Matarajio yasiyo ya kweli katika mahusiano,—yawe ya kibinafsi au ya kitaaluma,—yanaweza kusababisha matatizo makubwa. Utafiti mmoja uligundua kuwa wenza wenye matarajio makubwa walikuwa na uwezekano mkubwa wa kukumbwa na hali ya kutoridhika baada ya muda. Hii ni kwa sababu pengo kati ya matarajio na uhalisia husababisha migogoro na tamaa.
Kwa nini tunaweka matarajio yasiyo ya uhalisi
Kuelewa ni kwa nini tunaweka matarajio yasiyo halisi ni muhimu katika kuyadhibiti kwa ufanisi. Hapa nitataja sababu kadhaa ikiwemo kwanza, asili ya mwanadamu ya kuwa na matumaini mengi na makubwa.
Kiasili, wanadamu wana matumaini mengi, tukiamini kuwa • wakati ujao utakuwa bora zaidi kuliko wakati uliopita na tutafanikiwa zaidi. Matumaini yetu. Aghlab, huwa makubwa kuliko kuhalisia.
Sababu nyingine ya watu kuwa na matarajio makubwa yasiyo na uhalisia ni ulinganisho wa kijamii. Nadharia ya ulinganishi wa kijamii iliyotayarishwa na Leon Festinger (1954) inasema kuwa kwamba tunabaini uthamani wetu kulingana na jinsi tunavyojilinganisha na wengine. Katika enzi ya mitandao ya kijamii, ulinganisho huu ni wa mara kwa mara na mara nyingi husababisha matarajio yasiyo ya kweli kuhusu jinsi maisha yetu yanapaswa kuonekana.
Simulizi za hadith za kimapokeo na kiutamaduni pia zinachangia watu kuwa na matarajo makubwa kuliko uhalisia.• Jamii nyingine zina vigezo vya kimapokeo vya kuwa na mafanikio ikiwemo kupata kazi, gari, nyumba, shahada ya chuo kikuu na kadhalika, kuwa na kiasi fulani cha pesa katika umri fulani na kadhalika.
Matarajio haya ya jamii yanaweza kuleta shinikizo kwa mtu na kuweka malengo na matarajio makubwa kuliko uhalisia.
Mikakati mitano ya udhibiti wa matarajio
Kwa kuzingatia hatari za matarajio yasiyo halisi, tunawezaje kuyadhibiti kwa ufanisi? Hapa kuna mikakati mitano ya kuoanisha matarajio na ukweli au uhalisia.
Jambo la kwanza muhimuni kujifunza kuukubali ukweli kukubali ukweli jinsi ulivyo, badala ya jinsi tunavyotamani uwe. Kwa kujizoeza kukubali ukweli, tunaweza kupunguza maumivu mbalimbali ya kiakili yanayosababishwa na matarajio ambayo hayajatimizwa.
Hatua nyingine ni kuweka malengo yanayozingatia mafanikio ya kimchakato kuliko matokeo ya mwisho. Kwa mfano, badala ya kusema kuwa unakusudia kuweka akiba ya shilingi milioni 20 kwa mwaka, sema unalenga kuweka asilimia 20 ya pato lako kila mwezi.
Kingine unachoweza kufanya ni kudhibiti pengo la matarajio na kile kinachotokea. Ili kudhibiti pengo hili, rekebisha matarajio yako kulingana na hali halisi, kwa mujibu wa tathmini. Hii inaitwa kupatanisha matarajio na ukweli. Ikiwa ulitarajia kupata faida ya asilimia 10 kwenye uwekezaji, lakini utabiri unapendekeza asilimia 5, rekebisha matarajio yaendane na uhalisia.
Jambo jingine la kufanya ni kupunguza ulinganisho wa kijamii, hasa kupitia mitandao ya kijamii, ambayo aghlab, inaweza kuzidisha matarajio yasiyo ya kweli.. Ubaya wa mitandao ya kijamii ni kuwa inaweza kukufanya uhisi wewe peke yako ndio mwenye maisha magumu kwani kila umuonae anajisifu kwa hili au lile, akitangaza neema hii au ile aliyoipata.