
Nimepata hadhi hii kwa sababu ya kuacha yasiyonihusu
Kutoka kwa Anas bin Malik (Allah amridhie) amesimulia kuwa, mtu mmoja alifariki wakati wa Mtume (rehema na amani ya Allah zimshukie), mmoja wa watu waliokuwepo wakati anakufa akasema: “Pokea bishara njema ya Pepo,” akimaanisha huyo aliyekufa ni mtu wa Peponi.
Mtume (rehema na amani ya Allah zimshukie) akasema: “Hivi hujui? Huenda yeye (huyo aliyekufa) aliwahi kuzungumzia mambo yasiyomhusu, au alikuwa bahili kwa kitu kisichomtajirisha.” [Tirmidhi].
Tunayojifunza kutokana na tukio hili
Tusipeleleze mambo ya watu
Mara nyingi watu huvuka mipaka katika mazungumzo yao kwa kutozingatia mafundisho ya Uislamu kuhusu adabu za vikao na mazungumzo. Leo hii watu wengi hawachungi haki za wenzao pindi wanapozungumza na wala hawaoni aibu kuzungumzia masuala ya watu wengine.
Kitendo cha kuingilia au kuulizia mambo ya watu kinapingana na mafundisho ya Uislamu, ambayo yanalenga kuimarisha mafungamano mazuri baina ya watu katika ngazi ya familia, jamii na taifa; na pia kuweka mfumo imara unaojali haki za watu katika mambo maalumu yanayowahusu.
Mfumo huu unajikita katika kuweka mazingira mazuri kupitia adabu, tabia na maadili mema. Swahaba Mtukufu, Abi Huraira (Allah amridhie) ameripoti kuwa, Mtume (rehema na amani zimshukie) amesema: “Miongoni mwa uzuri wa Uislamu wa mtu ni kuacha yasiyomhusu.” [Sahih at–Tirmidhi hadith nambari 2317].
Hii ni kanuni inayolinda siri za watu na kutojiingiza katika kuwazungumzia.
Umakini katika mazungumzo
Ni jambo la kawaida sana kuwaona watu wanatumbukia kwenye dimbwi la matatizo na mizozo mikubwa kutokana na kauli zao. Haya ni matokeo ya watu kuacha mafundisho sahihi, kanuni na misingi tuliyowekewa na dini.
Mtume (rehema na amani ya Allah zimshukie) amesema: “Yeyote anayemuamini Allah na Siku ya mwisho azungumze maneno mazuri au anyamaze.” [Bukhari na Muslim]. Na katika musnadi yake, Imam Ahmad (Allah amrehemu) amenukuu hadith ya Mtume (rehema na amani zimshukie) inayosema: “Miongoni mwa uzuri wa Uislamu wa mtu ni kuwa na maneno machache katika mambo yanayomhusu.”
Iwapo Muislamu atazingatia mafunzo haya, ni dhahiri kuwa hawezi kujihusisha na mambo yasiyomhusu. Ujasiri anaoupata mtu wa kujiingiza katika mambo ya watu wengine unasababishwa na tabia ya kupenda kuchunguza kila jambo na kulizungumzia.
Ikiwa mtu atapunguza au kuacha kuzungumzia mambo yake binafsi, atajijengea utamaduni wa kuchunga na kuzingatia kile anachokisimulia na hatimaye atajiepusha na kuzungumzia mambo yasiyomhusu.
Minong’ono ya siri ndiyo chimbuko la tabia hii
Tabia ya kuzungumzia mambo ya watu inatokana na kupendelea mazungumzo ya siri. Ni mara chache sana mazungumzo ya siri baina ya watu wawili au zaidi yakasalimika na utesi (kusengenya) au kuzungumzia mambo ya watu wengine.
Ndiyo maana watu wengi hawazungumzi mambo yao ya siri hadharani na badala yake wanatafuta kificho kisha wanaanza kuzungumza. Allah ‘Azza Wajallah’ anasema: “Hakuna kheri katika mengi wanayoshauriana kwa siri isipokuwa kwa yule anayeamrisha kutoa sadaka, au kutenda mema, au kupatanisha baina ya watu. Na mwenye kufanya hayo kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu, basi tutampa ujira mkubwa.” [Qur’an, 4:114].
Kwa hiyo, tusipendelee kukaa kwenye vikao vya siri kwani ndiyo chanzo kikubwa cha kuwasengenya watu, kuwachonganisha, na pia kuzungumzia masuala mbalimbali ambayo hatuna uhusiano nayo.
Amru bin Qays al–Mulai (Allah amrehemu) amesema, kuna siku mtu mmoja alipita mahala alipokaa Luqman na watu wengine, akahisi kuwa Luqman amekuwa mtu mwenye hadhi na heshima kubwa kiasi cha kuzungukwa na watu, hivyo akamuuliza: “Wewe si ulikuwa mtumwa wa watu fulani?” Luqman akajibu: “Ndiyo.”
Yule mtu akamuuliza: “Nini kimekufikisha katika hali hii ninayoiona?” Luqman akasema: “Ni kwa sababu ya ukweli na kuyanyamazia yale yasiyonihusu.”