
Suhayl bin Amr, Mjumbe wa Makureish katika mkataba wa Hudaibiya
Jitihada zake kiibada na kujielimisha
Suhayl alijutia kuutumia umri wake mwingi ovyo na kwa aliyoyafanya kabla ya kusilimu. Hivyo basi, tangu aliposilimu, alijitahidi kufanya kila lililo katika uwezo wake kujikaribisha kwa Mola wake.
Inasemekana, hapakuwepo yeyote miongoni mwa waliosilimu kipindi hicho aliyemshinda kwa wingi wa ibada kama vile swala, funga za sunna, sadaka na kwa kusoma Qur’an.
Mkasa wake na Dhiraar
Suhayl (Allah amridhie) alijenga mazoea ya kumfuata Muadhi bin Jabal (Allah amridhie) kila siku kwa ajili ya kwenda kujifunza Qur’an.
Bwana mmoja akiitwa Dhiraar ibn al-Khattab akamwambia: “Ewe baba Zaid, mimi nakuona unakwenda kwa huyu jamaa wa Kikhazraj kujifunza Qur’an, kwa nini basi huendi kwa mtu yeyote katika watu wako (Muhajirina)?”
Akamwambia: “Ewe Dhiraar, haya uyasemayo ni katika athari za kikale (kijinga) sana, na haya ndio yaliyotuchelewesha (yaliyotubakisha nyuma) mpaka tukatanguliwa kwenye kheri.
“Na uelewe kwamba, Uislamu umekuja kukomesha un’gan’ganizi wa kikabila (wa kijinga) na kuwatukuza watu ambao hawakuwa na hadhi yoyote katika jamii (wengine wakabaki dhalili). Tunatamani lau tungelikuwa pamoja nao (walioukubali Uislamu mapema wakatukuzwa) tukatangulia kama walivyo wao.” [taz. Suwarun min hayat sahaba uk.536].
Baada ya kusilimu, maisha yote ya Suhayl bin Amr baada ya kusilimu maisha yake yaliongozwa na sharia za kiislamu. Kwa maana nyengine, aliutekeleza Uislamu katika kila kona ya maisha yake.
Aliwaonea tamaa sana waliomtangulia kusilimu na kuugundua ubora wao juu yake. Siku moja alikuja ofisini kwa Amirul Muuminina, Umar, akawakuta akina Alharith bin Hisham na Abu Sufian bin Harb (Allah amridhie), kisha wakaja wakina Amar bin Yasir, Suhaib Aroumy, pamoja na wengine miongoni mwa waliosilimu mapema wakateswa sana.
Akatoka mfanya kazi wa Umar akasema: “Haya, waingie Amar na Suhaib. Watu wakaangaliana kuonesha kutoridhika na upendeleo ule, wakasema: “Hatujapata kuona udhalili kama tulivyouna leo. Umar anawaruhusu hawa kuingia mwanzo bila ya kuzingatia uwepo wetu!?”
Suhayl akawaambia: “mkikasirika inatakiwa mujikasirikie (mujilaumu) wenyewe. Tulilinganiwa kama walivyolinganiwa, wao wakawahi kusilimu sisi tukajichelewesha, basi kuna kosa gani wao kuitwa mwanzo!? Na je itakuwa ajabu siku ya kiama wao watakapoitwa mwanzo kabla yetu!”
Suhayl akaendelea: “Wallahi kheri walizotangulia kuzipata (wenzetu) ni bora zaidi kuliko huku kututangulia leo hii kuingia katika ofisi ya Khalifa ambapo nyinyi mnagombeana hapa.” Kisha akasema: “Hawa wenzetu wametupita (wametutangulia) kwenye kheri, na wala hatuna namna ya kuipata kheri hiyo ila kwa kuipigania dini ya Mwenyezi Mungu na kufa Mashadidi.” [Taz. Suwarun min hayat sahaba uk.536-537].
Suhayl kushiriki jihadi
Wakati wa kipindi cha khalifa Umar, vita vilikuwa vimepamba moto katika ardhi ya Sham baina ya Waislamu na Warumi. Suhayl aliwakusanya wake, wanawe na wajukuu zake, akaondoka nao na kuelekea Sham, ili washiriki –kwa namna moja au nyengine- pamoja naye katika Jihad.
Aliwaambia: “Wallahi siachi jambo lolote nililolifanya dhidi ya Waislamu nilipokuwa na washirikina ila nitalifanya nikiwa dhidi ya washirikina, na gharama yoyote niliyoitoa dhidi ya Waislamu nitaitoa kama hiyo kwa ajili ya kuitetea dini ya haki.”
Akaendelea: “Naapa nitabaki katika mapambano kwa ajili ya dini ya Allah mpaka niuawe Shahidi, au nife nikiwa mbali na Makka.” Katika vita vya Yarmouk, Suhayl alionesha ukweli wa azma kwa kuonesha ushujaa mkubwa miongoni mwa wapiganaji Waislamu wa kupigiwa mfano.
Kifo chake
Suhayl bin Amr (Allah amridhie) aliendelea kushiriki katika harakati mbali mbali za kuikomboa Sham hadi mwaka wa 18 Hijriya sawa na mwaka 639 Miladiya enzi hizo hizo za utawala wa Umar ambapo ulizuka ugonjwa hatari wa tauni naye akawa miongon mwa waliofariki.
Maradhi hayo ya kuambukiza ambayo yaliitwa kwa jina la kitongoji yalipozuka (Amuwas) pia yaliwaua Maswahaba wengi na kila aliyekuwa naye miongoni mwa wake na watoto wake.
Tujifunzayo katika maisha ya Suhayl
Kuna mengi ya kujifunza katika maisha ya swahaba huyu mtukufu ikiwemo umuhimu wa kushikamana na aina mbali mbali za ibada, ikiwemo kujifunza, kuisoma na kuihifadhi Qur-an.
Muislamu haitakiwi kujitia shughuli nyingi mpaka akakosa muda wa kukisoma kitabu cha Allah. Na kama hajui kuisoma, aende kujifunza kwa wajuao, kama tulivyoona jinsi Suhayl alivyojitahidi na utu uzima wake kwenda kwa walimu kujifunza.
Tujifunze pia kwamba utukufu na heshima ya mtu ni kwa kumtambua Allah na kumuabudu kwa kuogopa adhabu zake huku akitarajia Pepo yake siku ya malipo. Utukufu haupimwi kwa mali, umaarufu, kabila wala rangi ya mtu.
Wakina Suheib Rumi, Amar bin Yasir, Bilal bin Rabah, Khabab bin Arat na kadhalika walitukuka kuanzia hapa duniani, kiasi cha kutangulizwa kuingia ofisi ya khalifa Umar walipopanga foleni mbele ya wakina Abu Sufian bin Harb ambao walikuwa mabwana wakubwa pale Maka.
imulizi pia inatufunza kwamba, mtu akiwa hajasilimu (akiwa kafiri) hutawaliwa na fikra chafu zikampelekea kujenga chuki dhidi ya wengine, na kufanya maamuzi yasiyoendana kabisa na utu.
Muangalie Suhayl bin Amr namna alivyomtesa mwanawe wa kumzaa pale aliposilimu wakati yeye ni mushrik bado, fikiria namna alivyokuwa mgumu wakati wa kuandika mkataba wa Hudaibiya, ambapo hakuruhusu hata majina ya Mwenyezi Mungu “Arrahman Arrahim” kuingizwa katika mkataba ule.
Kisha ona pale alipomuita mwanawe kwa aibu sana na kumuomba aseme na Mtume amsamehe yawmul fathi (siku ya kutekwa Makka). Bila shaka lile gwanda jeusi la ujahili lililomfunika Suhayl kwa muda mrefu lilikuwa limeanza kufunuka taratibu na kuuona mwanga wa dini na ubinadamu. Halafu na angalia pia uhalisia wa maisha yake baada ya kusilimu. Ama kweli Uislamu ni nuru na ukafiri ni giza.
Katika kisa cha Suhayl (Allah amridhie), kuna somo zuri kwa walinganiaji. Ni kutokuvunjika moyo na kumkatia tamaa unayemlingania kwa sababu ya ukaidi, ujabari na hila zake katika kuupinga Uislamu. Daawa ni ibada endelevu. Kazi ya mlinganiaji ni kufikisha tu, kuongoka ni kwa taufiki ya Allah.
Haikutarajiwa sana mtu kama Suhayl angelisilimu, na hiyo ndiyo iliyokuwa dhana ya wengi miongoni mwa maswahaba. Na ndio mana Umar alimuomba Mtume amruhusu kumuua Suhayl, pale alipoangukia mikononi mwa Waislamu (teka) katika vita vya Badr. Lakini baadae akasilimu. Allah awaridhie wote.