
Mapenzi ya kweli ni mlezi wa familia
Vichocheo vya mapenzi
Mume kumsaidia kazi mkewe
Kumsaidia mke kazi za nyumbani ni moja ya vichocheo vya mapenzi katika ndoa. Kazi kama vile kufua, kupika, kuosha au mume kujihudumia mwenyewe walau mara mojamoja, ni jambo jema na la kheri linalojenga mazoeano na kuzisogeza nyoyo za wanandoa.
Mume kusaidia kazi za nyumbani ni lugha ya kivitendo inayotafsiri kauli kama vile: “Nakujali”, “Nakuhurumia” na “Nakupenda sana mke wangu. Lugha ya mume kivitendo ni rahisi mke kuielewa, na yeye huijibu kwa maneno na vitendo: “asante mume wangu, najua unanipenda na mimi pia nakupenda.”
Kigezo chetu katika hili pia ni Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie). Maisha yake katika nyumba zake na wakeze kwa kweli yalikuwa ya kupigiwa mfano kule kuenewa na huruma na upendo.
Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alipenda kujishusha (kuwa mnyenyekevu) na kutoa msaada kwa alioishi nao ilimradi maisha yao yarahisike. Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alisema: “Mbora wenu ni mbora wenu kwa watu wake, na mimi ni mbora wenu kwa watu wangu.” [Tirmidhi].
Mama Aisha (Allah amridhie) alipoulizwa kuhusu shughuli za Mtume akiwa nyumbani kwake alisema: “Alikuwa akiwatumikia watu wake, wakati wa swala ukiingia hutoka kwenda msikitini kuswali.” [Bukhari].
Na katika mapokezi mengine Bi Aisha alisema: “Mtume alipokuwa nyumbani mwake alikuwa mpole kuliko watu wote, na alikuwa mkarimu kuliko watu wote, alikuwa ni mwanamume kama nyinyi, ila alikuwa mcheshi sana, na alikuwa binadamu kama bindamu wengine. Alikuwa akiwasaidia kazi watu wa nyumbani kwake, alikuwa akishona nguo yake mwenyewe, akitengeneza kiatu chake (kinapoharibika) akijihudumia, na alijishughulisha kama anavyojishugulisha mmoja wenu nyumbani mwake, ikiingia swala hutoka kwenda msikitini kuswali, na sikupatapo kumuona (wala kusikia) kwamba aliwahi kumpiga mwanamke au mtumwa kwa mkono wake.” [Ahmad].
Mazingatio
Huyu ndiye mwalimu na kiongozi wetu. Na hivi ndivyo anavyotakiwa awe kila mume Muislamu ndani ya nyumba yake. Ifahamike kwamba, mume katika nyumba ya ndoa si bwana kwa maana yake halisi na wengine wawe watumwa. La hasha, bali mume ni mtumishi wa familia na kiongozi wao.
Kwa hiyo, si vyema kwa mfano, mke kuhangaika jikoni akiandaa chakula kitakacholiwa na wote, huku mume amejilaza kitandani akichezea simu anasubiri kiwe tayari wale!
Ziko wapi hizo huruma na dalili za kumpenda mke wake? Mapenzi si maneno tu yajazwayo kinywani kisha yakatemwa. Kupenda kunataka kujituma kwa ajili ya kumridhisha umpendae! Uvivu si mtaji katika kuyachuma mapenzi.
Uelewa mbaya
Kuna baadhi ya wanaume hawafahamu umuhimu wa kuwasaidia kazi za nyumbani wake zao, kazi ambazo kusema kweli ni nyingi na ngumu. Hilo la kuwasaidia kazi na lililotosha kuwafanya wanawake wawapende waume zao.
Baadhi ya wanaume wanaamini kuwa kazi za ndani ni za wanawake, na wao kamwe haziwahusu. Na wale ambao wanajua kuwa wanaume pia wanaaswa kusaidia kazi za ndani, basi hulidharau jambo hilo na kutolifanya.
Hakuna aibu mume kushirikiana na mkewe kufua nguo zao. Sio uchuro mume kumsaidia mkewe kupika, kusogeza chakula au maji ya kunawa au kutandika busati wanapotaka kula. Wala si aibu kushika ufagio na kufagia. Na hayo hayampunguzii mume hadhi na nafasi yake kama kiongozi mkuu wa familia kwa sababu hayo hayo pia yamefanywa na Mbora wa Viumbe, Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie).
Kumuita kwa jina alipendalo
Mara tu baada ya kuoana, mke anatakiwa amfuatilie mume ni kwa jina gani anapenda amuite kama vile bwana, mume wangu, baba Fatuma, honey nk. Mume naye kwa upande wake, anatakiwa ampeleleze mke wake jina lipi anapenda amuite. Hili haifai kulidharau kwa kuwa ni moja ya vichocheo vya mapenzi.
Qur’an imeashiria haja ya mke kumuita mumewe “bwana” katika kisa cha Mtume Yusuf (Amani ya Allah imshukie) pale inaposema: “..basi wakamkuta bwana wake mlangoni..” hii ni ile kukuru kakara iliyotokea wakati Yusuf alipojaribu kumtoroka yule mwanamke aliyemtaka wafanye dhambi, na mwanamke akimfuata na kutaka kumzuia.
Bila shaka neno “bwana” hapa halijatumika kama kinyume cha “mtumwa” au “mjakazi” kwani mwanamke yule mle ndani hakuwa mjakazi wa waziri, bali alikuwa mke wake.
Na katika aya nyingine ndani ya sura hiyo hiyo, alitajwa kama “mraatul-aziz” (mke wa mheshimiwa waziri). Qur’an inasema: “Na wanawake wa mjini wakasema, ‘Mke wa waziri anamtamani kijana (mfanya kazi) wake kwa ajili ya nafsi yake, kweli ameathirika kimapenzi! Sisi hakika tunamuona yuko katika upotofu wa wazi.’” [Qur’an, 12:30].
Na mtu kumuita mwenzake kwa jina alipendalo ni katika mafunzo ya Mtume Muhamad (rehema za Allah na amani zimshukie) kwa mujibu wa hadith ya Umar aliyesema kuna mambo matatu huwa ni kielelezo cha mapenzi yako kwa nduguyo: kumsalimia unapokutana naye, kumwachia nafasi kwenye kikao na kumuita kwa jina alipendalo zaidi.”
Itaendelea In shaa Allah Kwa mrejesho wasiliana na mwandishi kwa namba 0773181494