Familia

Jenga moyo wa kukubali kukosolewa kwa kufanya haya

Kuwa kwenye uhusiano kunamaanisha kujifunza na kukua, na hayo hayatokei ila kwa kukubali kukosolewa na kurekebishwa.

Lakini tukubali ukweli—kukubali kurekebishwa, aghlab, si jambo rahisi. Mara nyingi, wengi wetu tukikosolewa hupenda kujitetea, kueleza sababu za matendo yetu, au kuhisi tunaonelewa na kuumia. Hata hivyo, moyo wa kujifunza ni muhimu kwa ndoa yenye afya na ustawi.

Lakini kiuhalisi, maneno ya kukukosoa na kukurekebisha kutoka kwa mwenzi wako siyo shambulio kwako bali mchakato wa ukuaji wa pamoja. Aghlab, ukosoaji na maneno ya ushauri na kurekebisha yanatokanana na upendo hivyo lengo si kukuvunja moyo bali kukufanya kuwa bora zaidi.

Kwa hivyo basi, unapokosolewa, badala ya kujibu kwa kiburi au kujihami, chukua muda kusikiliza. Jiulize, je, kuna ukweli katika kile anachosema mwenzangu? Hata kama kuna upungufu katika namna ya uwaslishaji, ujumbe wake unaweza kuwa mzuri na wa thamani.

Wataalamu wameshauri njia kadhaa zinazoweza kukusaidia kujenga moyo wa kukubali kukosolewa, kurekebishwa na kufunzika.

Badilisha mtazamo wako

Chukulia ukosoaji na marekebisho kama ishara ya upendo, na usichukulie kama shambulio. Hii inataka kubadilisha mtazamo hasi wa mambo kuwa chanya. Elewa kuwa marekebisho kutoka kwa mwenza wako hayakusudii kukudhuru, bali yanalenga kukusaidia kukua na kuwa bora zaidi.

Mosi, sikiliza bila kujihami na kuleta visingizio

Badala ya kujitetea, chukua muda kusikiliza na uelewe anachosema mwenzako. Kuwa mwepesi wa kusikiliza, si mwepesi wa kusema au kukasirika. Mwitikio wa kujihami hufunga mazungumzo yenye maana. Kiukweli, wakati mwingine ni bora kukubali tu makosa badala ya kutafuta visingizio visivyo na msingi.

Pili, kubali mapungufu yako na badilika. Ndiyo njia pekee ya ukuaji

Hakuna mtu mkamilifu. Kila mtu ana mapungufu yake. Kuwa na mapungufu hakupunguzi ubinadamu au heshima yako bali kunakamilisha utu wetu na kututofautisha na Muumba wetu, Allah aliye mkamilfu.

Hivyo basi, ukipata mtu anayekwambia makosa yako (badala ya kutangaza aibu zako kwa wengine) na kukutaka ujirekebishe, jua huyo ana upendo na unapaswa kumshukuru kwa kukusaidia. Kumbuka, kukua kunahitaji mtu kukubali mapungufu yake na kuwa tayari kujiboresha.

Tatu, dhibiti hisia zako kabla ya kujibu

Ni kawaida kuhisi kuumia au kuaibika unaporekebishwa, lakini vuta pumzi kabla ya kujibu. Kujielewa kihisia na kuweza kudhibiti hasira na mihemko yako hukuwezesha kupeleka mrejesho bila kulichukulia suala hilo kama shambulio la kibinafsi, lenye nia mbaya na hatimaye kukufanya ulipuke kwa hasira.

Nne, omba ufafanuzi badala ya kumdhania mtu vibaya

Hata dini imekataza dhana kwani dhana hupelekea uongo. Badala ya kuweka dhana mbaya kwa mwenzi wako kuwa anakushambulia, muulize, “Unaweza kueleza unachomaanisha?” Hii inasaidia kuhakikisha unaelewa vizuri mtazamo wake badala ya kuingiza dhana na hatimaye kupotosha anachosema.

Bahati mbaya wanawake ndiyo mahiri sana katika dhana na kupotosha. Mume anaweza kusema tupunguze matumizi kwa sababu hali ngumu, lakini mke akajibu “Kwa hiyo mi ndo mfujaji namaliza ela zako humu ndani?”

Tano, epuka kukasirika, kununa, kususia au kufunga mawasiliano

Baadhi yetu tuna tabia ya kukasirika, kununa, kususa kwa sababu tumekosolewa na wenza wetu. Haipaswi kuwa hivyo. Kurekebishwa hakumaanishi ujitenge au usiongee. Badala ya kufunga mawasiliano, eleza hisia zako kwa utulivu na kwa njia ya kujenga.

Sita, tekeleza marekebisho na uonyeshe ukuaji

Marekebisho hayana maana ikiwa hayatapelekea mabadiliko ya kiutendaji na kitabia. Jitahidi kuboresha maeneo ambayo mwenzi wako anakuelekeza kwa upendo, vinginevyo itamkatisha tamaa na kuacha kukwambia tena lolote analoona linaenda kombo.

Saba, onesha shukrani kwa uwazi wa mwenzi wako

Thamini ukweli kwamba mwenzi wako anajali ukuaji wako kwa kumwambia. Kauli rahisi kama “Asante kwa kunieleza kwa kuwa muwazi” inaweza kusaidia sana kumpa moyo aendelea kukushauri maeneo ya kurekebisha katika maisha yenu na hivyo kuimarisha uhusiano wenu.

Nane, kurekebishana iwe pande zote

Hamasishanei kukosoana na kurekebishana wa pamoja (pande zote mbili) na uwajibikaj ili kujenga uhusiano wenye afya. Mweleze mwanandoa mwenzako kuwa uko tayari kupokea maoni yake na vile vile kutoa maoni yako ya kujenga inapohitajika. Wakati mkifanya hivyo, msisahau nafasi ya kila mtu: Mume kama kiongozi na mke msaidizi, hivyo heshima ni muhimu. Mwisho, Muombe Mungu akupe hekima na unyenyekevu wa kupokea ukosoaji kwa njia nzuri. Moyo wa kujifunza hujenga uhusiano wenye mafanikio. Wakati wenzi wote wanapokubali kurekebishwa kwa upendo na unyenyekevu, wanatengeneza mazingira salama ya ukuaji, uaminifu, na uhusiano wa kina zaidi.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button