Dkt. Zakir Naik, gwiji wa da’awah ya Kiislamu duniani
Dkt. Zakir Abdul Karim Naik ni mwanazuoni na mlinganiaji wa Kiislamu kutoka nchini India, ambaye amebobea katika fani ya Dini Linganishi (Comparative Religion).
Dkt. Naik ni Muasisi na Rais wa taasisi ya Islamic Research Foundation (IRF) na televisheni mashuhuri ya Peace TV. Ni mtu maarufu sana katika ulimwengu wa Kiislamu.
Mara kadhaa Dkt. Naik amekuwa akidai kuwa yeye siyo mfuasi wa itikadi yoyote ya madhehebu za Uislamu, lakini inaonesha wazi kwamba yeye ni mwanasunna, tena wa kiwango cha juu.
Maisha ya awali na elimu
Zakir Naik ni mtoto wa Mzee Abdul Karim Naik na Bi. Roshan. Alizaliwa mwezi Oktoba mwaka 1965 huko Bombay nchini India, jiji ambalo kwa sasa linaitwa Mumbai.
Alijiunga na Chuo cha Kishinchand Chellaram kisha akasomea udaktari wa binadamu (medicine) katika Chuo cha Topiwala National Medical College & BYL Nair Charitable Hospital. Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Mumbai ambako alihitimu shahada ya kwanza ya Tiba na Upasuaji (Medicine and Surgery).
Kazi zake
Dkt. Naik alianza kufanya kazi ya da’awah mwaka 1991. Miezi michache baadae akaanzisha shule ya Kimataifa ya Kiislamu jijini Mumbai na Shirika la Misaada la Kiislamu linalojulikana kama United Islamic Aid, ambalo linatoa udhamini wa masomo kwa vijana wa Kiislamu masikini na wasiojiweza. Mke wa Dkt. Naik, Farhat Naik ni Rais wa Kitengo cha Wanawake cha Taasisi ya Islamic Research Foundation (IRF).
Dkt. Naik alipata msukumo wa kulingania Uislamu kutoka kwa Sheikh Ahmed Hussein Deedat, mhubiri mashuhuri wa Kiislamu wa Dini Linganishi kutoka Afrika Kusini, ambaye alikutana naye mwaka 1987.
Wakati mwingine Dkt. Naik anarejelewa kama ‘Deedat plus’, yaani nyongeza ya Deedat, lakabu ambayo alipewa na Sheikh Deedat mwenyewe.
Januari 21, 2006, taasisi anayoiongoza ya Islamic Research Foundation ilianzisha televisheni mashuhuri ya Kiislamu inayoitwa Peace TV. Televisheni hii kubwa duniani iliyo na makao makuu yake huko Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) inarusha matangazo yake kwa njia ya satelaiti bila malipo.
Televisheni hiyo ambayo inarusha maudhui ya Kiislamu imepigwa marufuku nchini India, Bangladesh, Canada, Sri Lanka na Uingereza kwa kisingizio cha kusambaza matamshi ya chuki (hate speech), jambo ambalo si la kweli.
Katikati ya mwezi Machi 2021, Dkt. Naik alizindua mtandao wa ‘Al Hidaayah’, ambao unatoa maudhui ya kielimu kuhusu Uislamu. Jukwaa hili la kimtandao lina maelfu ya video za wazungumzaji wa Kiislamu zaidi ya 40 ulimwenguni kote, akiwemo Sheikh Ahmed Deedat, Yusuf Estes, Hussein Ye, na Dkt. Bilal Philips. Dkt. Naik anadai kwamba jukwaa hili ni toleo ‘halali’ la Netflix.
Mihadhara na midahalo
Tofauti na wahubiri wengi wa Kiislamu, mihadhara ya Dkt. Naik ni ya mazungumzo ya kawaida yanayotolewa kwa lugha ya Kiingereza, siyo Kiurdu wala Kiarabu, na mara nyingi huvaa suti ya Kimagharibi na tai. Dkt. Naik ametoa mihadhara mingi na kufanya midahalo mingi mno ulimwenguni kote.
Thomas Blom, mtaalamu wa Anthropolojia kutoka Sweden ameandika kwamba, mtindo wa Dkt. Naik wa kuhifadhi Qur’an na hadith za Mtume katika lugha mbalimbali na shughuli zake za kida’awah, zimemfanya kuwa mtu maarufu sana katika duru za Waislamu.
Midahalo yake mingi imerikodiwa na kusambazwa kwa upana kwa njia ya DVD na mtandaoni. Mazungumzo yake yamerikodiwa kwa lugha ya Kiingereza na kurushwa kwenye mitandao kadhaa ya ‘cable’ jijini Mumbai na kwenye chaneli ya Peace TV. Mada anazotoa zaidi ni pamoja na Uislamu na Sayansi, Uislamu na Ukristo, na Uislamu na Usekula.
Ukuu wa Uislamu
Ndugu zangu katika imani, si rahisi kumuelezea Dkt. Naik kwa ukamilifu kupitia makala moja tu. Nguli huyu wa da’awah amefanya midahalo mingi na kutoa mihadhara mingi sehemu nyingi tofauti duniani, ikiwemo katika vyuo vikuu mashuhuri na vyenye heshima kubwa.
Katika moja ya nukuu zake, Dkt. Naik amesema:
Uislamu ndiyo dini bora kwa sababu Qur’an inasema hivyo. Hakuna maandiko yoyote (mengine) ya kidini yanayodai ukweli huu.
Aliongeza kuwa, Uislamu pia umebandikwa lebo ya kutokuwa na ‘uvumilivu’, na kwa kweli hauna ‘uvumilivu’ dhidi ya ufisadi, ubaguzi, dhuluma, zinaa, ulevi na uovu mwingine wote. Uislamu ni dini yenye ‘uvumilivu’ mkubwa pale suala la kukuza maadili ya kibinadamu linapohusika.
Masuala ya kijamii
Dkt. Naik analinganisha muziki na ulevi ambapo amesema kwa asili yake, vyote viwili vinalevya. Anapinga kucheza muziki na kuimba kwa sababu mambo yote hayo yamekatazwa katika Uislamu.
Dkt. Naik anasema, wale waliotiwa hatiani kwa makosa ya wizi waadhibiwe kwa kukatwa mikono. Pia anapendekeza Marekani itekeleze adhabu hii ili kupunguza viwango vikubwa vya uhalifu nchini humo. Dkt. Naik anasema, jamii ya mashoga na wasagaji (LGBT) ina ugonjwa wa akili unaosababishwa na matumizi ya picha chafu (ponography) yanayokuzwa na televisheni na mitandao ya kijamii.
Ukosoaji wa vyombo vya habari
Dkt. Naik amevitaja vyombo vya habari kama nyenzo muhimu sana, lakini ni silaha hatari zaidi duniani inayoweza kugeuza nyeusi kuwa nyeupe na kumfanya muovu kuwa shujaa. Anashauri kutumia vyombo vya habari kuondoa dhana potofu, nukuu potofu, tafsiri potofu na upotoshaji wote unaofanywa dhidi ya Uislamu.
Dkt. Naik anasema, ikitokea mwanamke wa Kiislamu amevaa hijab au niqab, hiyo inaitwa udhalilishaji wa wanawake, lakini mtawa akifanya hivyo inageuka na kuitwa dalili ya heshima na adabu!
Mwanaume Muislamu mwenye umri wa miaka 50 akimuoa binti wa miaka 16 kwa (ridhaa yake) inakuwa habari kubwa kwenye vyombo vya habari, lakini mwanaume asiye Muislamu mwenye umri wa miaka 50 akimbaka binti wa miaka sita inakuwa habari ndogo tu ya kujazia!
Utasikia wanasema kwenye vyombo vya habari kwamba Uislamu unawanyima haki wanawake na ni dini isiyofaa kabisa. Wanautuhumu Uislamu kuwa ndiyo tatizo kubwa kwa wanadamu hapa duniani ingawa ukweli ni kwamba Uislamu ndiyo suluhisho pekee la matatizo yote ya wanadamu!