Darsa za wiki

Ibada kama njia ya kudumisha amani, mshikamano wa kidini

Kila ibada katika Uislamu ina hukumu za kisheria zilizowekwa kwa mujibu wa matini thabiti katika Qur’an na Sunna. Allah amewajibisha kwa waja wake ibada mbalimbali kwa malengo mahususi, ikiwemo kuwajumuisha watu pamoja, kuwafanya wawe na hali na msimamo mmoja na kuepuka mifarakano na mizozo.

Ukiangalia nguzo tano za Uislamu, hupati tabu kutambua chanzo na msingi mkuu wa nguzo hizo kuwa ni umoja. Mfano, nguzo ya kwanza ambayo ni kukiri kuwa hakuna anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah pekee, na kwamba Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani iwe juu yake) ndiye Mtume wake, ni Shahada ambayo hutolewa na Waislamu wote, popote walipo duniani na wakati wowote.

Na kupitia nguzo ya pili, sala, Waislamu huelekea upande mmoja (Qibla) kwa namna moja wakimuabudu Mola Mmoja; wakati katika ibada ya swaumu ya Ramadhan, Waislamu wa ulimwengu mzima hufunga mwezi mmoja kwa namna moja wakijizuia mambo mbalimbali yaliyokatazwa.

Kwa upande wa zaka, Waislamu waliotimiza vigezo na masharti ya kutoa kiasi fulani (Nisab) cha pesa, mifugo, mazao ya nafaka, dhahabu au fedha, wameagizwa kuwapa sehemu ya mali zao wale wanaostahiki kwa wakati maalumu.

Hata hivyo, mfano mkubwa zaidi wa umoja katika Uislamu ni ibada ya Hijja, ambapo Waislamu hutoka kila kona duniani na kuelekea nchi moja wakivaa mavazi yanayofanana (Ihram) huku wakimuomba Mola Mmoja.

Kwa hakika, Uislamu umeweka sheria na ibada kwa lengo la kuitakasa nafsi na kuisafisha kutokana na maovu na shari, na kumfanya mwanadamu awe na cheo cha juu kabisa na hatimaye awe ruwaza na mwangaza kwa wengine. Muislamu anatakiwa aishi katika jamii yake kwa amani, usalama na umoja, na kuwatahadharisha watu juu ya hatari ya kusambaratika.

Sala na mshikamano

Ibada katika Uislamu zinasisitiza na kuelekeza kwenye umoja na mshikamano. Kwa mfano, sala ina athari kubwa katika kuunganisha jamii ya Kiislamu katika hali ya usawa wa kiwiliwili na kimoyo.

Katika ibada ya sala, Waislamu husimama kwenye mistari sawa bila ya ubaguzi wala upendeleo. Hairuhusiwi Muislamu yeyote kujiona bora kuliko mwingine kwa sababu ya rangi, jinsia au nafasi aliyonayo. Pia, katika kuhakikisha umoja, mshikamano, ushirikiano, usawa na umoja baina ya Waislamu, sala ya jamaa imefanywa kuwa bora kuliko sala anayoiswali mtu peke yake.

Licha ya kutofautiana kwa makabila, lugha, utamaduni, rangi na utaifa, Waislamu wanatakiwa kushikamana na kuungana. Ni mshikamano ambao, kupitia ibada kama sala, ndiyo unaupa nguvu na ustawi Uislamu katika misingi na malengo yake, hatimaye umma unaondokana na unyonge, udhaifu na kufarikiana.

Mwenye nguvu amsaidie mnyonge, tajiri amfadhili masikini, mdogo amheshimu mkubwa na mkubwa amhurumie mdogo. Hayo yote yanatokana na ukweli kuwa Waislamu wote ni ndugu wenye uhusiano imara wa kuhurumiana, kupendana na kusaidiana. Allah Mtukufu anasema: “Hakika Waumini ni ndugu.” [Qur’an, 49:10].

Kwa kweli, kusali pamoja msikitini kuna thawabu adhimu zilizobainishwa na Mtume (rehema za Allah na amani iwe juu yake) aliposema: “Sala ya jamaa ni bora kuliko sala ya mtu peke yake kwa daraja 27.” [Bukhari na Muslim].

Zaka kichocheo cha huruma, mapenzi

Hali ni hiyo hiyo katika ibada ya zaka ambayo inawaelekeza Waislamu kwenye umoja, ushirikiano na kuondoa hitilafu. Ibada ya zaka kimsingi, ni mfumo wa kifedha na kijamii, na pia ni mojawapo ya nguzo za dini na faradhi zake kuu.

Ibada ya zaka inamlea Muislamu na kumuandaa kuwa mja mwenye kumtakasa Allah peke yake na kuwa mwanadamu mwenye manufaa kwa jamii yake. Aidha, Allah Aliyetukuka ametaja utoaji wa zaka kama mojawapo ya sifa za Waumini aliposema: “Na (Waumini ni wale) ambao wanatoa zaka” [Qur’an, 23:4].

Pia, zaka ni ibada inayosaidia kuleta umoja baina ya Waislamu, hivyo ni sharti na ni muhimu mno waihifadhi na kuitekeleza barabara. Hii ni ibada inayowaunganisha matajiri na masikini.

Kutoa huchochea hisia za huruma katika nyoyo za matajiri na hivyo kuwafanyia hisani na kheri masikini. Isitoshe, zaka inasababisha matajiri na masikini kuheshimiana na kupendana kutokana na kile ambacho matajiri wanawapa masikini katika mali zao.

Funga na Hijja

Swaumu (funga) iko hivyo hivyo kama tulivyotaja sala na zaka. Swaumu, siyo tu inaathiri mwenendo wa wafungaji bali pia ni sababu ya muungano wa umma na mshikamano wake.

Vilevile, swaumu inachangia sana kuwaelekeza Waislamu washikamane, washirikiane na wahurumiane wenyewe kwa wenyewe. Pia, swaumu inamfanya Muislamu amuonee huruma ndugu yake.

Yaliyotajwa kuhusu sala, zaka na swaumu ni yale yale yasemwayo kuhusu hijja, ibada ambayo inakutanisha mamilioni ya Waislamu kutoka pande zote za dunia bila kujali tofauti za rangi, makabila, utaifa au maeneo wanayotoka. Ibada ya hijja inadhihirisha umuhimu wa umoja na muungano wa Waislamu kwa ajili ya kumtakasa Mola Mmoja kwa wakati mmoja, sehemu moja na kwa namna moja. Hivyo ni sahihi kusema kuwa, ibada ya hijja inaleta umoja pengine kuliko ibada nyingine yoyote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button