Kimataifa

Taasisi za Kiislamu Uingereza zalalama kubaguliwa ‘kifedha’ kisa ugaidi 

Zaidi ya asilimia 40 ya mashirika ya Kiislamu nchini Uingereza yamekatishiwa huduma zao za benki, ripoti mpya ya Muslim Charities Forum (MCF) imebaini.

Ripoti hiyo, iliyotolewa wiki hii na kuripotiwa na Middle East Eye, imeeleza kuwa mashirika ya Kiislamu yanakabiliwa na “ubaguzi mkubwa wa kifedha, unaohusiana moja kwa moja na sera za kupambana na ugaidi na mifumo ya tathmini ya hatari.”

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, asilimia 68 ya mashirika ya Kiislamu yalikiri kupata ugumu katika kufungua akaunti za benki, huku asilimia 42 yakiripoti kufungiwa kabisa huduma zao za kifedha. Aidha, mashirika manne kati ya 10 yalishuhudia ucheleweshaji mkubwa wa uhamishaji wa fedha, jambo lililowaathiri katika kulipa mishahara na kugharamia huduma muhimu. Shirika moja linaloendesha hospitali limesema kuwa halikufanikiwa kuwalipa madaktari na wauguzi wake kwa muda wa miezi miwili, hali iliyoathiri huduma za afya kwa jamii inayotegemea hospitali hiyo.

Katika kisa kingine, shirika moja linalofanya kazi Mashariki ya Kati limesema ucheleweshaji wa kutuma fedha ulisababisha watoa huduma kufika kwenye ofisi zao za uwanja wakiwa na silaha wakidai malipo, na hivyo kuhatarisha maisha ya wafanyakazi wao.

Ripoti hiyo imeeleza kuwa Waislamu ndio jamii inayochangia zaidi katika misaada ya kibinadamu nchini Uingereza, lakini mashirika yao yanakumbwa na kile kinachoitwa “de-banking” na “de-risking,” hali inayowafanya kupoteza fedha na huduma za kifedha kwa misingi isiyoeleweka.

Abdulsami Arjuman, Mkuu wa Sera na Utetezi wa MCF, ameeleza kuwa tatizo hili limekuwa likiathiri mashirika ya Kiislamu kwa zaidi ya miongo miwili. “Hata hivyo, pamoja na umuhimu wa suala hili, bado halijapewa uzito unaostahili,” alisema.

Arjuman alitaka mifumo ya kifedha ifanywe kuwa na uwazi zaidi, kuwe na ulinzi wa kutosha kwa mashirika haya, na benki kuwajibika ipasavyo ili kuzuia kuadhibu mashirika ya Kiislamu bila sababu za msingi.

Ripoti hiyo iliongeza kuwa “Uislamofobia wa kimfumo” umekuwa chachu ya mashirika haya kunyanyaswa kifedha bila ushahidi wowote wa uhalifu. Kesi nyingi zimeripotiwa, ikiwemo ile ya mwaka 2019 ambapo Middle East Eye ilifichua kuwa World Uyghur Congress ilizuiliwa kutuma fedha kwa misingi ya propaganda za China, zilizoituhumu kimakosa kama kundi la kigaidi. Vilevile, Msikiti wa Finsbury Park jijini London ulishuhudia akaunti yake ikifungwa kwa madai yasiyo na msingi ya kuhusika na ugaidi. Ripoti hii inakuja miezi michache baada ya mwanasiasa mashuhuri Nigel Farage kuripoti kufungiwa akaunti zake za benki bila maelezo, na kuvutia vyombo vya habari kuandika habari hizo kwa ukubwa. Hata hivyo, mashirika ya Kiislamu nchini humpo yamekuwa yakikumbana na changamoto kama hii kwa muda mrefu bila hatua yoyote ya maana kuchukuliwa ili kutatua tatizo hili sugu.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button