
Asilimia 80 ya Waislamu Ujerumani wamewahi kubaguliwa
Wanafunzi Waislamu nchini Ujerumani wamekutana jijini Frankfurt kwa mkutano wao wa kila mwaka kujadili changamoto za kijamii, huku suala la ubaguzi dhidi ya Waislamu likipewa uzito mkubwa.
Kikao maalum kuhusu ubaguzi wa rangi kilichoongozwa na wataalamu wa sheria kilibainisha kuwa Waislamu wanakabiliwa na ubaguzi mkubwa katika sekta mbalimbali za maisha nchini humo.
Kwa mujibu wa uchambuzi uliofanyika katika mkutano huo, asilimia 87 ya washiriki walikiri kuwa wamewahi kukumbana na ubaguzi wa rangi katika mazingira ya shule, vyuo vikuu, sehemu za kazi na maeneo ya umma. Hali hii inathibitishwa na utafiti wa 2023 wa shirika la “Claim Allianz,” ambalo liligundua kuwa karibu asilimia 80 ya Waislamu au watu wanaochukuliwa kuwa Waislamu nchini Ujerumani wamepitia matukio ya ubaguzi.
Taasisi za haki za binadamu zinaeleza kuwa Waislamu katika jamii za Magharibi mara nyingi hukumbana na ubaguzi unaotokana na mwonekano wao, asili yao ya kitamaduni, na imani yao ya kidini.
Hali ikiwa hivyo, wanawake Waislamu wanakabiliwa na changamoto zaidi kutokana na ubaguzi wa kijinsia. Wataalamu wanatahadharisha kuwa ubaguzi wa rangi husababisha kutengwa kwa jamii na katika hali mbaya zaidi, unaweza kuchochea matukio ya ukatili dhidi ya Waislamu.
Pamoja na uzoefu wa ubaguzi unaowakumba Waislamu wengi duniani, hakuna mwanafunzi yeyote kati ya waliokuwepo kwenye mkutano aliyewahi kuripoti rasmi tukio la ubaguzi. Wataalamu walihimiza waathirika wa ubaguzi kuripoti matukio hayo kupitia ofisi rasmi kama vile Ofisi ya Kupambana na Ubaguzi nchini Ujerumani. Viongozi wa Kiislamu walisisitiza kuwa vita dhidi ya ubaguzi vinahitaji hatua za taasisi na jamii kwa ujumla, wakizitaka mamlaka, waajiri, na umma kwa ujumla kushirikiana kuhakikisha haki na usawa vinazingatiwa kwa jamii zote.