Latest

Mzee Mwinyi Aasa Wasomi Waliopikwa Al-Azhar Sharif

NA MWANDISHI WETU

Kutoka kulia, Sheikh Ismail Mohammed, Sheikh Ally Khamis Ngeruko mjumbe wa Baraza la Ulamaa, Sheikh Alhad Mussa Salum, Sheikh Assayid Awadh Abdulazim mudiri wa Markaz, Rais mstaafu Ali Hasani Mwinyi, Sheikh Yakubu Mrisho Lubela, Rais wa Umoja wa wahitimu wa Al-Azhar Sharif, Makamu wa Rais mstaafu, Dkt Gharib Bilal na Sheikh Zailai Mkoyogole.

Rais mstaafu wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi amewataka Waislamu nchini kudumisha umoja miongoni mwao na kuepukana na mitafaruku isio na tija. Akizungumza na Waislamu katika sherehe zilizoandaliwa na Umoja wa Wahitimu wa Al-Azhar Sharif, tawi la Tanzania kwa kushirikiana na Kituo cha Kiislamu cha Kimisri cha Dar es Salaam Mwinyi alisema hali ya kufarakana imechangia kurudisha nyuma maendeleo ya Waislamu. “Ni muhimu Waislamu wakawa na umoja miongoni mwao kwani mifarakano inazorotesha Uislamu katika nyanja zote,” alisema Mzee Mwinyi. Kwa upande wake Makamu wa Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Gharib Bilali aliwahimiza Waislamu kuwa chachu ya kudumisha amani na kuwa kitu kimoja. Akizungumzia suala la ulianganiaji, Sheikh Abdallah Haruna, Mjumbe wa Umoja wa Wahitimu wa Al-Azhar Sharif tawi la Tanzania na Imamu wa Msikiti wa Kiblateni, Kariakoo Dar es Salaam, alisema kuwa ni vema Waislamu wakafuata njia alizokuwa akizitumia Mtume Muhammad (rehema na amani ya Allah ziwe juu yake) katika ulinganiaji. Naye, Sheikh Asayid Awadh Abdulazim Mudiri wa Markaz ya Kimisri aliwashukuru waandaji wa sherehe hizo huku akiwataka waendelee kudumisha umoja miongoni mwao. Akizungumza kwa niaba ya Umoja wa Wahitimu wa chuo cha Azhari Sharrif, Yakub Mrisho Lubela ambaYe pia ni Rais wa Umoja huo alisema kuwa ni muhimu kwa viongozi wa kisiasa na kidini kusaidia ili umoja huo uendelee kusonga mbele. “Tunaomba nyie viongozi wetu wote wa kidini na kisiasa mzidi kusaidia umoja huu udumu kwa michango yenu ya hali na mali,” alisema Mrisho.

About Admin