Latest

Masheikh Wajitosa Sakata La Madawa Ya kulevya

Wakati mapambano ya dawa za kulevya hapa nchini yakizidi kushika kasi, baadhi ya masheikh wamepongeza na kuunga mkono vita hiyo, na kushauri vita hiyo iendeshwe kwa tahadhari. Mmoja wa masheikh hao, Kaimu Katibu Mkuu wa taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Sunna Tanzania (BASUTA), Muhammad Issa alisema kuwa hatua zilizochukuliwa kukabiliana na janga hilo ni za kupongezwa na kila Mtanzania. Hata hivyo, Sheikh Muhammad Issa alisema kuwa mapambano hayo yaendeshwe kwa tahadhari ili kuepuka kuwahusisha na kuwaonea wasiohusika. “Mchakato huu usitumike kuwaonea watu, kwa visasi kwa kuona hii ndiyo fursa kuwasingizia wengine na kusababisha wakamatwe, kama ilivyo kwa kesi za watuhumiwa wa ugaidi ambazo watu hukaa mahabusu muda mrefu,” alisema Sheikh Muhammad. Akielezea msimamo wa Uislamu kuhusu madawa ya kulevya, Sheikh Muhammad alisema: “Mafundisho ya Waislamu yanaharamisha kila aina ya kilevi bali inapokuja kwa Serikali wao ni vilevi vya aina fulani ila dawa za kulevya ni mpaka sigara.”

Sheikh Ponda

Kwa upande wake, Katibu wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda amesema kuwa athari zitokanazo na matumizi ya dawa za kulevya ni kubwa hivyo ni lazima kuwepo mjadala wa kitaifa utakaowahusisha viongozi wa dini na watu wengine muhimu ili kupata suluhu ya kudumu. “Kwa mujibu wa Uislamu dawa za kulevya ni haramu kwa kuwa yanapelekea kudhuru mwili. Hivyo ni wajibu kwa viongozi wa Kiserikali na dini kuzuia na kuwakemea watu wanaojihusisha na uuzaji pamoja na matumizi ya dawa za kulevya,” alisema Sheikh Ponda. Ili kupata suluhu ya kudumu, Sheikh Ponda ameishauri serikali ipige marufuku matumizi ya vilevi vyote badala ya kutumia muda mwingi katika kushughulikia dawa za kulevya pekee.

Sheikh Kundecha

Naye Amiri wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Mussa Kundecha, amesema kuwa suala la dawa za kulevya halina mjadala kwani ni biashara haramu. “Uislamu hauna mjadala wa biashara za dawa za kulevya kwani ni vitu haramu, tatizo ni uregevu wa sheria mahali popote ndiyo unaofanya kiwango cha uhalifu kuwa kikubwa,” alisema Sheikh Kundecha. Sheikh Kundecha aliongeza: “Angalia duniani kote inapotumika sheria ya Mwenyezi Mungu hata kiwango cha uhalifu ni kidogo nani kwa sababu ni sheria inayoendana na maumbile ya mwanaadamu.” Pia Sheikh Kundecha aliongeza kuwa hata pombe nazo zipigwe marufuku na kukosoa maelezo ya kuwepo kwa pombe pombe haramu na baadhi eti zikiitwa kuwa ni za halali. “Unaposema pombe ni haramu, halafu ukasema kuna pombe halali basi hata ile unayoita haramu nayo ushaihalalisha. Hivyo ni vema Serikali ikapiga marufuku pombe zote, kwani hata Uislamu unasema kuwa kila kilicho kuwa haramu hakiwezi kuwa biashara,” alisema Sheikh Kundecha. Maoni ya Watanzania Gazeti la Imaan lilipata pia fursa ya kuongea na baadhi ya Watanzania wa kawaida akiwemo Juma Kilanga aliyesema kuwa hatua zinazochukuliwa sasa na Serikali zinapaswa kuungwa mkono na kila Mtanzania ili kutokomeza kabisa biashara hiyo haramu. “Madawa haya yameharibu vijana wengine sana hapa nchini, hivyo inampasa kila Mtanzania kuhakikisha anaunga mkono vita hii kwa dhati ili kuhakikisha inakoma,” alisema Kilanga. Naye Said Itura mkazi wa Dar es Salaam alisema kuwa ni aibu kuona kuna majina mengi ya Waislamu huku akipendekeza kuwa watakaothibitika kuhusika na biashara hiyo wachukuliwe hatua kali za kisheria. “Halafu inatia aibu ukiangalia katika orodha hii ya dawa za kulevya majina ya Waislamu ni yamo mengi sana, hili halikubaliki. Masheikh wana wajibu wa kuelimisha umma juu ya athari za dawa hizi na biashara yake,” alisema Itura. Itura pia alishauri Serikali iwasake wote wanaojihusisha na dawa za kulevya, na watakaothibitika kuhusika wachukuliwe hatua kali, bila kujali sura ya mtu au hadhi yake katika jamii,” alisema Said Itura. Naye Barnabas John mkazi wa Dar es Salaamu alisema kuwa vita hii ya dawa za kulevya ni vita kubwa sana inayohitaji mbinu nyingi ili kuweza kukabiliana nayo. “Hii vita ni kubwa, kwani mtandao wa biashara za kulevya ni wa Kimataifa, hivyo ni vema mamlaka husika zikatumia mbinu nyingi ili kukabiliana nayo.”.

Mapambano yalivyoanza

Hivi karibuni Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alitangaza majina ya baadhi ya watu mashuhuri ambao wanadaiwa kujihusiha na dawa za kulevya na kuwataka wafikie Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam. Hadi gazeti hili linakwenda mitamboni zaidi ya watu 100, wakiwemo watu maarufu tayari walishafika na kuhojiwa huku baadhi wakitarajiwa kufikishwa mahakamani. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alionesha uungaji mkono wake vita hiyo na kusema mapambano hayo yasijali mwanasiasa wala mtu maarufu na kwamba kila anayehusika akamatwe. “Tembea kifua mbele katika vita hii ya dawa za kulevya, hakuna mtu maarufu, hakuna mwanasiasa, hakuna askari, hakuna waziri au mtoto wa fulani ambaye anajihusisha aachwe. Hata kama angekuwa mke wangu Janeth, shika tu kwa sababu dawa za kulevya kwa taifa letu sasa zimefika mahali pabaya,” alisema Rais Magufuli. Tanzania inafuata mfano wa nchi nyingine duniani zilizoamua kupambana na dawa hizo ikiwemo Ufilipino ambako Rais wa nchi hiyo, Rodrigo Durtete aliamua kutumia jeshi la n kupambana na biashara hiyo haramu.

About Admin