Hapa na Pale

RC Mtanda: Wataalamu wa ununuzi zingatieni maadili, weledi

Wataalamu wa sekta ya ununuzi wa umma wametakiwa kuzingatia weledi na maadili ya taaluma ya fani yao katika usimamizi wa miradi ya umma ili kuiwezesha Serikali kupata thamani halisi ya fedha katika miradi yake.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda ametoa raia hiyo katika hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masala wakati wa kufunga mafunzo ya Moduli ya uwasilishaji na ushughulikiaji wa malalamiko na rufaa (Complaint and Appeal Management Module) katika Mfumo wa Ununuzi wa Umma kwa njia ya Kieletroniki (NeST).

Mtanda alisema, kuzingatia maadili ya taaluma ya fani hiyo katika usimamizi wa miradi siyo tu kutaiwezesha Serikali kupata thamani halisi ya fedha bali kutaiheshimisha fani ya ununuzi na ugavi pamoja na Serikali.

“Nendeni mkatumie elimu hii kuwaelimisha wengine ili waweze kuielewa na kuitumia moduli. Naamini ninyi mlioshiriki mafunzo ya awamu hii mtakuwa mabalozi wazuri wa moduli hii na PPAA kwa ujumla,” alisema Mtanda.

Naye Katibu Mtendaji wa Mamlaka ya Rufaa za Zabuni za Umma (PPAA), James Sando, alisema baada ya Serikali kujenga mfumo wa Ununuzi wa Umma kwa njia ya Kieletroniki (NeST) na kuweka sharti la lazima kufanya ununuzi wa umma katika mfumo huo, PPAA ilishirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kujenga moduli ya kuwasilisha na kushughulikia malalamiko na rufaa kieletroniki ili kuwawezesha wadau wa ununuzi wa umma kuwasilisha malalamiko na rufaa zao kieletroniki.

Aliongeza kuwa washiriki wa mafunzo hayo wamejifunza moduli ya uwasilishaji na ushughulikiaji wa malalamiko na rufaa, ambayo inajumuisha maeneo ya uwasilishaji wa malalamiko kwa Afisa Masuhuli wa taasisi nunuzi iliyotangaza zabuni. Mafunzo hayo ya siku tatu yamefanyika jijini Mwanza kuanzia Februari 4 hadi 6 na kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 580 kutoka mikoa ya Mwanza, Geita, Mara, Kagera, Simiyu na Shinyanga.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button