Hapa na Pale

Rais Samia ataja changamoto tatu majengo Kariakoo

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema ajali ya kuporomoka kwa jengo katika soko la Kariakoo imetoa somo jinsi biashara inavyoendeshwa ndani ya majengo mengi katika soko hilo.

Rais Samia amebainisha hayo Ikulu jijini Dar es Salam wakati wa hafla ya chakula cha mchana pamoja na wadau walioshiriki kazi ya uokozi baada ya jengo la ghorofa kuanguka Kariakoo mnamo Novemba 16 mwaka jana.

Katika hotuba yake, Rais Samia alitaja changamoto kubwa tatu alizoziona katika majengo yaliyopo katika soko hilo kuwa ni pamoja na majengo mengi kuzidiwa na uzito wa mizigo.

“Tumeelezwa jengo lilikuwa na uwezo wa kuchukua tani 250 za mizigo lakini tani zilizokuwa pale ni 850, kwa hiyo kwa vyovyote lisingeweza kubeba na hilo ni jengo moja. Nina hakika majengo mengi yaliyopo Kariakoo yapo katika mfumo huo,” alisema Rais Samia na kuongeza:

“Utanuzi wa majengo unafanywa kwa msingi uleule uliopo mwanzo na si kuanza upya, tunarefusha juu, tunachimba chini lakini kwa msingi uleule , hii ni hatari.”

Rais alitaja changamoto nyingine kuwa ni usimamizi hafifu wa serikali wakati wa ujenzi katika kuhakikisha viwango vya ujenzi vinazingatiwa. “Usimamizi wa serikali wakati wa ujenzi na kuhakikisha viwango vya ujenzi unafuatwa, kwa tulioliona jengo tulikuwa tunaona mchanga mwingi kuliko saruji,” alisema.

Aliongeza kuwa ajali ya Kariakoo imeonesha mambo mengi, likiwemo suala la uwepo wa mali ambazo hazilipiwi kodi. “Mimi nililiona kwa haraka haraka na pengine huleta mzozo ni mali inayofichwa mle ndani na pengine bila kulipiwa kodi. Sidhani kama zile tani 850 zimelipiwa kodi na ndio ulikuwa ugomvi mkubwa kwa TRA wanapopeleka watu kukagua maghala ndani ya Karikaoo,” alifafanua Rais Samia.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button