
Kicheko wanaojifungua watoto njiti, baba siku 7 za kulea
Serikali imeridhia hoja ya kuongeza muda wa likizo ya uzazi kwa mwajiriwa ambaye atajifungua mtoto njiti kwa kujumuisha na muda uliobaki kufikia wiki 40 za ujauzito huku baba akipewa siku saba za mapumziko.
Kwa muda mrefu wadau mbalimbali wamekuwa wakipigia chapuo hoja hiyo ili kulinda ustawi na afya za watoto wanaozaliwa kabla ya wakati ambao wanahitaji muda wa kutosha wa uangalizi wa mama.
Akiwasilisha bungeni maelezo ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Kazi Namba 13 wa Mwaka 2024, kwa niaba ya Waziri wa Nchi – Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde alisema, awali katika Muswada ilipendekezwa muda wa wiki 36 kama ukomo wa muda wa mtoto kutimia.
Hata hivyo, alisema baada ya majadiliano na kamati, serikali ilikubaliana na mapendekezo ya kuongezwa muda huo hadi kufikia wiki 40 na kuongeza muda wa likizo ya baba ambaye atapata mtoto njiti kuwa siku saba badala ya tatu. Akisoma maoni ya Kamati ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Fatma Toufiq alishauri serikali kuona namna ya kufanya maboresho katika sheria ili kuruhusu pia wanaojifungua watoto wenye mahitaji maalum kama vile usonji, vichwa vikubwa, mgongo wazi, mdomo sungura, matundu kwenye moyo, seli mundu kupewa likizo maalum ya uzazi pindi wanapojifungua.