
Wapeni motisha walimu wa madrsa – wito
Sheikh wa Wilaya wa Kinondoni, Mohammed Ahmed Muhenga, amewataka Waislamu kutoa motisha kwa walimu wa madrasa, akisisitiza kuwa kazi wanayoifanya ni kubwa kiasi ambacho hata wakilipwa kiasi gani cha pesa, hakiwezi kulingana na thamani ya wanachofanya.
Sheikh Muhenga ametoa rai hiyo katika mashindano ya Qur’an yaliyoandaliwa na Madrsat Swiratal Mustaqima Islamic Center ya Mwananyamala, Dar es Salaam chini ya usimamizi wa Sheikh Jumanne Mtiga na Ofisi ya Bakwata ya wilaya ya Kinondoni.
Sheikh Muhenga alisema atakayeshikamana na Qur’an, atafanikiwa katika maisha yake kwani atakuwa ameshikamana na mwongozo sahihi wa maisha yake, na hivyo alitaka walimu wa Qur’an wathaminiwe.
Kwa upande wake, Meya wa Wilaya ya Kinondoni, Mstahiki Meya Songoro Hamis Mnyonge ambaye alikuwa mgeni rasmi, alitoa rai kwa Waislamu kushikamana na Qur’an kwani ndio katiba ya Uislamu.
Wakati huo huo, Sheikh Musa Kundecha ambaye alihudhuria hafla hiyo alisema kuwa, anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuileta Qur’an duniani na kuifanya kuwa muongozo wa Waislamu.
“Hakika Qur`an ni mfumo kamili wa maisha ya mwanadamu, imeelezea kila kitu katika haya maisha na kuwaelekeza Waislamu namna bora ya kuitumia Qur`an kwa kumleta mwalimu, naye si mwingine ni Mtume Muhamad (rehema za Allah na amani zimshukie),” alibainisha Sheikh Kundecha.
Mashindano hayo yameshirikisha vipengele vya Juzuu 1, Juzuu 3, Juzuu 5, Juzuu 7, Juzuu 15 na Juzuu 30.
Washindi juzuu ya kwanza kuanzia namba moja ni Ahmad Abdulrahman, Mohammad Mussa, na Aiman Athuman. Juzuu 3 washindi ni Hamid, Sabiha Mohammed na Shadya.
Kwa upande wa Juzuu 5, washindi ni Bakari, Abubakar Suleiman, na Muhidin Swalehe huku katika juzuu 7 washindi wakiwa ni Mohamad Abdallah, Rahfa Lugobola na Fauzia Ally.
Juzuu 15 washindi ni Fahdi Jumaa, Abeid Majid na Mohamad Bilal huku katika juzuu 30 vinara wakiibuka Sumaiya Shuayb, Ismail Yusuf, na Suleiman. Washindi hao wa mashindano hayo yaliyobatizwa “Usiku wa Qur`an” yakiwa yamefanyika kwa mara 17 walipewa zawadi mbalimbali.