
Urais wa Trump wawapa hofu Waislamu Marekani
Wakati Donald Trump akijiandaa kuapishwa kuwa Rais wa Marekani Januari 20, Wamarekani wa asili ya Kiarabu na Kiislamu wanatafakari kwa kina kuhusu mustakabali wa sera za Marekani, hasa ikizingatiwa historia yake ya kuunga mkono kwa dhati Israel na manyanyaso dhidi ya raia wa mataifa yenye idadi kubwa ya Waislamu.
Trump, anayejulikana kwa msimamo wake mkali, mwaka 2017, aliwahi kutoa agizo lililozuia watu kutoka mataifa saba yenye Waislamu wengi kuingia Marekani. Hatua hiyo ilizua taharuki kubwa miongoni mwa Waislamu wa Marekani, huku ikitajwa na wakosoaji kuwa ni jaribio la “kupiga marufuku Waislamu.”
Hali kama hii inaibua hofu kwamba ahadi zake za kampeni za urais za 2024 za kurejesha na kupanua marufuku hiyo zinaweza kuchochea ubaguzi zaidi dhidi ya jamii hizo.
Katika jiji la Dearborn, Michigan, lenye idadi kubwa zaidi ya Waislamu Marekani, baadhi ya Wamarekani wa asili ya Kiarabu, walionekana kumuunga mkono Trump kwa matumaini ya sera zinazodhaniwa kuleta “amani kwa nguvu.”
Hata hivyo, wengine walionyesha shaka kuhusu utawala wake mpya, wakikumbuka kwamba utawala wake wa awali, haukuwa na uwazi kuhusu mwelekeo wa sera zake za Mashariki ya Kati.
Kwa upande mwingine, mzozo unaoendelea Gaza umeibua hasira miongoni mwa Waislamu wa Marekani. Shirika la Amnesty International limeeleza kuwa mashambulizi yanayoendelea huko Gaza yanaweza kufasiriwa kama “mauaji ya halaiki.” Wakati Trump akisema Israel lazima ishinde vita hivyo, wengi wanaona ukimya wa Marekani kuhusu haki za binadamu kama sehemu ya tatizo linalochochea mzozo wa Mashariki ya Kati badala ya kuutatua. Je, urais mpya wa Trump utakuwa ni mwendelezo wa hali hiyo, au kutakuwa na mabadiliko? Wakati utasema.