
Samia azindua sera mpyaya elimu, yaja na mapya
Baada ya mchakato wa muda mrefu, hatimaye Rais Samia Suluhu Hassan amezindua Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 toleo la mwaka 2023, huku akitaja mambo matatu yalimsukuma kutaka kufanyika mapitio ya sera baada ya kuingia madarakani.
Akizungumza jana jijini Dodoma, alisema licha ya kwamba ndiye aliagiza kufanyika kwa mapitio hayo, kazi kubwa ilishafanywa na watangulizi wake na ndiyo ilimfanya kuona kuna haja ya kufanyika kwa mapitio haya ili elimu inayotolewa iendane na kasi ya maendeleo ya teknolojia.
Alisema: “Nimesimama kwa fahari juu ya mabega ya walionitangulia kwa sababu wao ndio walinijengea jukwaa linalonifanya mimi nione mbele. Huko mbele ninaona dunia inayobadilika kwa kasi sana, mabadiliko ambayo ni sawa na upepo unaovuma kwa kasi unaweza kutupepea au kutupeperusha.
“Upepo huo ni kasi ya mabadiliko ya teknolojia ya habari na mawasiliano katika kujifunza au kuiharibu jamii, hivyo kutokana na upepo huo aliona ni lazima tuwe na maandalizi ya kufanya upepo utupepee na usitupeperushe. Mbele yetu pia ninaona mahitaji makubwa ya ajira kwa vijana ambayo yataendelea kuongezeka mbele ya safari kwa sababu kubwa tatu,” alisema.
Alizitaja sababu hizo ni kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia itakayosababisha baadhi ya kada nyingine kukua na nyingine kutoweka.
Sababu ya pili ni utandawazi ambao unatoa fursa ya bidhaa na huduma kutoka sehemu moja ya dunia kwenda nyingine kwa njia rahisi na bila kulazimika kuwa na msimamizi.
Pia, ongezeko la idadi ya watu lisiloendana na kasi ya ukuaji wa uchumi ni sababu nyingine iliyomsukuma Rais Samia kutaka mapitio hayo ya sera na mitaa. “Ukuaji wa asilimia 3.2 kwa mwaka inakadiriwa kwamba ifikapo mwaka 2044 idadi ya watu hapa nchini itakuwa milioni 123 na hivyo kuongeza uhitaji wa kazi na ajira kwa vijana, hivyo ninachokiona huko mbele kinatufanya tuwe na maandalizi ya kutosha kwa kuinua ubora wa elimu yetu,” alisema.
“Kwa kutoa elimu bora zaidi ya kisasa na kuandaa vizuri zaidi vijana wetu ili waweze kumudu stadi muhimu zitakazowawezesha kuajiriwa au kujiajiri. Elimu itakayowafanya vijana wetu waweze kushindana kikanda na kimataifa, kuwajengea ujasiri kuweza kujiamini. Kwa kufanya hivyo tutakuwa tunaandaa mazingira mazuri ya upepo kuwapepea vijana wetu badala ya kuwapeperusha.”
Rais Samia alisema miongoni mwa mambo muhimu yatakayoangaliwa ili kufanikisha utekelezaji wa sera na mitalaa hiyo ni mapitio ya maslahi ya kada ya ualimu nchini. Hatua hiyo inalenga kuipa hadhi inayos t a h i l i kada hiyo a m b a y o ndiyo mama wa taaluma zote, akieleza kuwa mwalimu ndiye kiungo wa utekelezaji wa sera na mitalaa.
“Kwa maoni yangu ndiye kiongozi wa elimu, hivyo katika maboresho haya lazima mwalimu awe katikati ya mduara wa maboresho yaliyofanyika na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kuajiri walimu wenye sifa na kuwapa mafunzo stahiki ili waendane na mwelekeo wa sera hii,” alisema.
“Aidha, tutapitia upya maslahi ya kada ya walimu nchini ili kuipa hadhi inayostahili kama mama wa taaluma zote duniani,”alisema.
Ataka PPP kwenye elimu
Katika kuhakikisha rasilimali fedha zinapatikana za kutosha, Rais Samia aliziagiza Wizara ya Fedha, Wizara ya Mipango na Uwekezaji, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kuwezesha na kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sera na mitalaa mipya ili kuleta matokeo yaliyokusudiwa.
“Sera ni nzuri, yaliyolengwa ndani ni makubwa, Serikali peke yake hatutaweza na kutegemea wahisani peke yao hatutaweza, dunia inabadilika, kila nchi ina changamoto zake, lakini tukienda na sekta binafsi tunaweza kufanya vizuri. Kwa hiyo tufanye maandalizi ya kwenda pamoja na sekta binafsi,” alisema Rais Samia.
Yaliyomo katika sera
Rais Samia alisema elimu itakuwa ya lazima kutoka miaka saba na kuwa 10 na kwamba ilitokana na wanafunzi kumaliza elimu ya msingi wakiwa na umri wa miaka 13 na hivyo kukosa sifa ya kuajiriwa na kujiajiri, huku hawana elimu ya ufundi na kwa sasa kupitia sera hiyo itamwezesha kijana kuingia kwenye uzalishaji.
Aidha, alisema sera hiyo inajibu hoja ya muda mrefu ya kuweka mfumo wa kutoa na kurasimisha ujuzi unaopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu na mafunzo uliopo. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alisema sera hiyo itawezesha kubadilisha mfumo wa elimu ili kuzalisha nguvukazi yenye ujuzi wa teknolojia.