
Masheikh wamkumbuka kwa mema Sheikh Muhammad Idd
Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir amesema kifo cha aliyekuwa Imam wa Msikiti wa Mnyamani Sheikh Muhammad Idd Muhammad kimeacha pengo kubwa katika jamii ya Kiislamu akisisitiza kuwa alikuwa ni shujaa, mpiganaji, jemedari na aliyekuwa tayari kujitoa kwa ajili ya wengine.
Akizungumza katika msikiti wa Mnyamani, Mufti Zubeir amekiri kuwa kuondoka kwa Sheikh Muhammad Idd kumehuzunisha watu wengi ndani na nje ya mipaka ya Tanzania kutokana na harakati zake za kulingania watu.
Sheikh Muhammad Idd, maarufu kama Abu Idd, alifariki asubuhi ya Alhamisi, Januari 30, 2025 katika Hospitali ya Mlonganzila alikopelekwa baada ya presha yake kupanda na alizikwa Ijumaa, Januari 31, 2025 huko kijijini kwao Mkata mkoa wa Tanga.
“Tumepata pengo katika Uislamu. Wengi wanafahamu jinsi alivyosimama. Alikuwa ni mtu wa kushirikisha wasomi katika mambo yake,” alisema Mufti Zubeir.
“Alikuwa anafika ofisini au kwa Sheikh Yusuph ambaye ni mwalimu wake na kutafuta ushauri, ndipo hapo alikuwa anakwenda kuendesha vipindi vyake, sio mtu wa kukurupuka,” alisema.
Sifa hii ya kushirikisha watu katika mambo muhimu kama haya sio ya kila mtu. Hakika tutamkumbuka kwa weledi wake na uhodari wake wa kuwasilisha mada. Alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha jambo lake linafika kwa umma na likaeleweka,” aliongeza Sheikh Zubeir.
Pia, Mufti Zubeir alimsifu Sheikh Muhammad Idd kwa utii wake kwa viongozi waliomzidi, “Alikuwa ni mtu ambaye yupo tayari kutumwa na kufikisha ujumbe mbele za umma na ukafurahi, kwa kweli alikuwa ni mtu mwenye kipaji kikubwa.”
“Kupitia kipindi chake cha Al-Rissala kilikuwa kinafuatiliwa na watu wengi. Faida kubwa imepatikana kutokana na kazi hiyo ya elimu aliyokuwa akiifundisha kupitia vyombo vya habari,” alisema Sheikh Zubeir.
“Dunia inafananishwa na mzoga ambao juu wapo mbwa wanaugombea, sio kitu cha thamani cha kukikumbatia, kila mtu afahamu kuwa ni safari ya watu wote. Hakuna kinachobaki cha msingi ni kuenzi yale yote mazuri yalikuwa yakifanywa na kumuombea kwa Mwenyezi Mungu apate malipo mema,” alisema Sheikh Zubeir.
Rais Hay-atul ulamaa afunguka
Kwa upande wa Rais wa Jumuiya ya Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania (Hay-tul ulamaa), Sheikh Abdallah Ndauga, amesema Sheikh Muhammad Idd alikuwa ni mmoja wa Waislamu ambaye alishiriki kikamilifu katika masuala ya kijamii na kulingania watu dini.
Alisema, alianza kumsikia siku nyingi sheikh huyo kupitia vyombo vya habari, na kwamba kwa muda mrefu ameweza kudumu na kazi hiyo ya kuhabarisha watu kuhusu suala la dini kupitia vipindi mbalimbali.
“Sheikh Muhammad namfahamu kama sheikh, mwenye juhudi katika dini, amekuwa ni mtu wa dini maisha yake yote. Nimemuona katika mihadhara mbalimbali ya dini. Ni mtu ambaye ametoa mchango mkubwa katika dini,” alisema alisema Sheikh Ndauga.
Viongozi wa kitaifa waguswa, watoa pole kwa umma wa Kiislamu
Watu wengi wameguswa na msiba wake akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliyetoa salamu za pole kwa Mufti na Waislamu kwa Ujumla.
Kupitia mitandao yake ya kijamii, Rais alisifu kazi nzuri iliyokuwa ikifanywa na Sheikh Muhammad Idd Muhammad ya kulingania umma wa Kiislamu.
“Tumeondokewa na mtu aliyeipenda nchi yake, mwalimu katika imani, mlezi wa wengi katika imani, mpenda haki, mpenda ukweli, umoja, amani na utulivu wa nchi yetu, aliyetumia muda wake mwingi kuyasimamia na kufundisha hayo kupitia mawaidha yake” Rais Samia alisema hayo kupitia mitandao ya kijamii
Aidha, Rais Samia alimuombea dua kiongozi huyo:“Mwenyezi Mungu ampe kauli thabit, amsamehe makosa yake, amzidishie katika mizani mema aliyotenda, na ampe nafasi katika Pepo yake,” palisomeka katika moja ya kurasa zake za mitandao ya kijamii
Mufti Kenya nae atoa neno, aguswa
Mbali na Rais Samia, mwingine aliyeonesha kuguswa na msiba wa kiongozi huyo ni Mufti wa Kenya Sayyid Ahmad Ahmad Badawiy Jamalullay ambaye alimuelezea marehemu kuwa ni mtu ambaye alipenda kazi ya ulinganiaji
Sheikh Sayyid Ahmad Ahmad Badawiy, kupitia kipande kifupi cha video alionesha kusikitishwa kwake na kifo cha kiongozi huyo na kusema kuwa ni hasara kubwa imepatikana kwa kuondokewa mwanachuoni huyo. “Sheikh Muhammad ameitikia wito. Hii ni amri na hakuna wa kuipinga. Yeye alikuwa ni maarufu, mkwasi wa kuarifiwa kwa juhudi zake. Alikuwa anatetea akida za Kiislamu. “Yeye ni msomi wa dini, alisoma kwa masheikh mbalimbali, mfano Sheikh Mahammad Ayub wa Tanga, ni mtu ambaye alihifadhi dini vizuri na kuitumikia Kwa kweli, kumkosa Sheikh Muhammad ni hasara kwetu, alikuwa ni mtu ambaye hajivungi katika kuweka mambo sawa, akiona kuna jambo haliko sawa la ki-akida,” alisema Sheikh Sayyid Badawiy.