
Mapigano DRC yaacha kiliokwa wafanyabiashara Tanzania
Mapigano yanayoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia Congo (DRC) yametajwa kuathiri biashara kati ya Tanzania na nchi hiyo, huku Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tatoa) kikiiomba Serikali kuwapatia ulinzi ili waweze kushusha mizigo na kurudisha magari yaliyokwama nchini humo.
Inaelezwa kuwa malori karibu 100 yakiwa na shehena za mizigo yaliyotoka hapa nchini yamekwama DRC, huku mengine yakishindwa kuvuka mpaka kutokana na hali ya usalama ilivyo.
Athari zaidi
Taarifa za Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Wakimbizi (UNHCR) zinaeleza zaidi ya watu 400,000 wamekimbia makazi yao tangu mwanzoni mwa mwaka huu kutokana na mapigano nchini DRC.
Pia, mashirika ya misaada yalisema kuwa hospitali zimefurika mamia ya watu waliojeruhiwa katika mapigano, wakiwemo watoto, huku Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) likisema usambazaji wa misaada ya chakula umesitishwa kwa muda ndani na karibu na mji wa Goma kutokana na mapigano hayo.
Vifo vya wanajeshi DRC
Katika mkutano wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc), uliofanyika juzi jijini Harare, Zimbabwe, viongozi hao walitoa salamu za pole kwa mataifa yaliyopoteza wanajeshi wake kwenye misheni ya kulinda amani (SAMIDRC) nchini DRC.
“Mkutano huo ulitoa salamu za rambirambi kwa nchi za DRC, Malawi, Afrika Kusini na Tanzania kwa wanajeshi waliopoteza maisha katika mashambulizi ya hivi karibuni huko Sake, Mashariki mwa DRC, wakiwa kwenye misheni ya SAMIDRC na wamewatakia waliojeruhiwa kupona haraka,” ilieleza taarifa rasmi ya viongozi hao baada ya mkutano wao juzi. Alipotafutwa ili kuzungumzia salamu hizo kwa Tanzania, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax alisema: “Naomba ongea na Waziri wa Mambo ya Nje
” Waziri wa Mambo ya Nje, Mahmoud Thabit Kombo hakupatikana mara moja wala kujibu ujumbe mfupi aliotumiwa, alipotafutwa kwa njia ya simu kuzungumzia suala hilo.
Mwananchi lilimtafuta pia Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi Mindi Kasiga ambaye pia alisema swali hilo aulizwe Waziri. Hata hivyo, Kasiga hakuwa na uhakika kama waziri huyo alikuwa amerejea nchini baada ya mkutano wa Harare. Hata hivyo, Balozi Kasiga ameahidi kutoa taarifa rasmi baada ya kuwasiliana na viongozi wake kuhusu suala hilo.
Hali ilivyo kwa sasa
Baada ya kuuteka mji muhimu wa Goma, waasi wanaotajwa kuungwa mkono na Rwanda wanaendelea kusonga mbele kuelekea kusini, katika hatua inayotishia makabiliano kati ya Rwanda na Burundi. Huko Bukavu, raia wanaandikishwa kulinda mji. Jeshi la DRC kwa msaada wa Jeshi la Burundi lilionekana likidhibiti shinikizo la waasi wanaoungwa mkono na Rwanda wanaotaka kupanua udhibiti wao wa mikoa ya mashariki mwa DRC katika mashambulizi ya wiki chache yaliyosababisha hofu ya mgogoro mpana wa kikanda.
Kwa mujibu wa Shirkika la Habari la Ujerumani (DW), waasi wa M23 waliiteka Goma, mji mkubwa zaidi mashariki mwa DRC ambao ni nyumbani kwa migodi ya dhahabu, coltan na madini ya shaba.
Waasi hao sasa wanaelekeza macho yao Bukavu, mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kusini na wanapiga hatua kuelekea lengo hilo huku matamanio yao yakiwa kuikamata Kinshasa.
Hata hivyo, Jeshi la DRC (FARDC) na washirika wake wamefanikiwa kuwadhibiti waasi hao, vyanzo vitatu, akiwemo Gavana wa Kivu Kusini, Jean-Jacques Purusi Sadiki vililiambia Shirika la Habari la Reuters.
Mmoja wa watu waliokuwa na taarifa za moja kwa moja kuhusu mapigano hayo, alisema kikosi cha takribani wanajeshi 1,500 wakiwemo wa DRC, Burundi na wanamgambo wa ndani, kilitumwa kulinda mji wa Nyabibwe ulioko kilomita 50 kaskazini mwa Bukavu. Wakazi wa Bukavu, ambao mara ya mwisho waliangukia mikononi mwa waasi mwaka 2004, walisema watu walikuwa wanajitayarisha kwa chakula, tochi na betri au kukimbilia mpakani mwa Burundi.
Raia walioajiriwa na mamlaka kutetea mji huo walikuwa wakifanya mazoezi kuzunguka uwanja wa michezo na kujipanga kwa ajili ya salamu za kijeshi.
“Tumeumia kwa muda mrefu kwa sababu ya wavamizi ambao ni majirani zetu,” alisema mwalimu wa hesabu Habamungu Mushagalusa, mmoja wa kundi la watu takribani 200 walioajiriwa kwa ajili ya kulinda.
“Tuko hapa kulinda ardhi yetu hadi kifo.” Rwanda imepinga matokeo ya wachunguzi wa Umoja wa Mataifa kwamba imetuma maelfu ya wanajeshi na vifaa nchini DRC kuisaidia M23.
Umoja wa Mataifa ulisema Alhamisi iliyopita kwamba kulikuwa na taarifa za vikosi vya Rwanda kuvuka mpaka na kuelekea Bukavu na Rwanda haijajibu ripoti hizo.