Habari

Kidato cha pili Kirinjiko wabuni kifaa cha kutambua ujazo wa maji

Wanafunzi wa kidato cha pili wa shule ya sekondari ya Kiislamu ya Kirinjiko iliyopo wilayani Same, mkoani Kilimanjaro wamebuni kifaa cha kidijitali cha kutambua kiwango cha maji yaliyohifadhiwa katika matenki au mabwawa.

Ubunifu huo ni matokeo ya kuanza kutolewa kwa mafunzo ya amali shuleni hapo mara baada kuanza kutumika kwa Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 Toleo la Mwaka 2023.

Akizungumza na dira ya habari jijini Dodoma katika banda la maonesho la shule hiyo, Mkurugenzi wa Kituo cha Kirinjiko Islamic Center, Mfaume Kihongosi amesema kuwa mafunzo ya amali yamekuwa na faida kubwa katika kuwaandaa vijana kukabiliana na changamoto ya ajira

Uzinduzi wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 Toleo la Mwaka 2023 ulifanyika jijini Dodoma mwishoni mwa wiki na ulizinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan ambapo alisema kuwa watashirikisha sekta binafsi ili kufikia malengo ya sera hiyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule hiyo, Mohammed Makini, amesema kuwa katika kuteleza sera hiyo upande wa mafunzo ya amali watazidi kuwaanda wanafunzi kuwa wabunifu ikiwa ni pamoja kuboresha kifaa hicho cha upimaji maji ili kuweze kukidhi mahitaji.

Mmoja wa wanafunzi waliobuni kifaa hicho, alitoa wito kwa wanafunzi wengine hasa watoto watoto wa kike kutokata tamaa na badala yake wajikite katika kubuni vitu mbalimbali kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.

Shule ya Sekondari Kirinjiko ni shule pekee ya Kiislamu iliyaoalikwa katika uzinduzi huo ambapo maonesho ya kielimu yalishirikisha takribani taasisi 17 za kielimu.

Wakati huohuo, baadhi ya wakuu wa taasisi za elimu zilizo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wamesema kuwa uzinduzi wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 Toleo la Mwaka 2023 utakwenda kukuza uchumi hapa nchini

Wakizungumza na Tv Imaan kando ya ukumbi ulipofanyika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu nchini (TEA), Dkt. Erasmus Kipesha, amesema taasisi yake imejipanga kuboresha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia mafunzo ya amali kama sehemu ya kuunga mkono utekelezaji wa sera hiyo.

Naye Katibu Mtendaji wa Baraza Mitihani la Taifa (NECTA), Dkt Said Mohamed amesema kuwa wameshajipanga vyema ili kuanza kutekeleza mtaala unaoakisi sera hiyo ambapo kwa mwaka huu darasa la pili watafanya mtihani wa kujipima hasa katika KKK (Kusoma, Kuandika na Kuhesabu).

Naye Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), Dkt Amani Makota amesema kwa upande wao wamefanya mageuzi makubwa kutokana na maelekezo ya sera hiyo ambayo alisema ikitekelezwa itainua uchumi. Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Profesa Charles Kihampa amesema kuwa nao wameshaanza kufanya maboresho ya mitaala ili kuzalisha wahitimu wenye ujuzi kutokana na maono ya sera hiyo.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button