6. Kutoka Katika Quran na Sunnah

Sayansi Mamboleo na Mafunzo Mbalimbali Ambatanishi

SEHEMU YA 7 Allah aliyetukuka anasema: “Na hakika katika wanyama wa mifugo kuna funzo kwenu. Tunakunywesheni katika yale yaliyomo matumboni mwao yaliyo baina ya kinyesi na damu; (nayo ni) maziwa safi yenye ladha nzuri kwa wanywaji. Na katika matunda ya mitende na mizabibu mnafanya humo vinywaji vikali vya ulevi (vinavyokatazwa) na riziki nzuri. Hakika katika hayo, bila shaka ni Aya (ishara, dalili, zingatio) kwa wanaotia (mambo) akilini.

“Na Mola wako alimtia ilhamu nyuki kwamba, jitengenezee nyumba katika majabali, na katika miti, na katika wanavyojenga (wanadamu). Kisha kula katika kila matunda, na fuata njia za Mola wako zilizofanywa nyepesi (kuzipita). Kinatoka katika matumbo yao kinywaji cha rangi mbali mbali ndani yake mna shifaa (ya magonjwa) kwa watu. Hakika katika hayo, bila shaka ni Aya (ishara, dalili, zingatio) kwa watu wanaotafakari.” (Qur’an, 16, 66-69). Mpenzi msomaji, katika makala iliyopita tulizungumzia muujiza wa kisayansi unaohusiana na maziwa kama nilivyoonesha Aya hapo juu. Na leo hii tutazungumzia aya inayofuatia katika katika sura hiyo hiyo ya 16 Aya ya 66-69 inayosema: “Na katika matunda ya mitende na mizabibu mnafanya humo vinywaji vikali vya ulevi (vinavyokatazwa) na riziki nzuri. Hakika katika hayo, bila shaka ni Aya (ishara, dalili, zingatio) kwa wanaotia (mambo) akilini”. Mpenzi msomaji, katika Aya hii, Allah anataja matunda ya aina mbili; tende na zabibu kuwa ni riziki nzuri: ‘Rizqan Hasanan’. Allah kayasifia matunda haya mawili kuwa ni rizki nzuri. Hii ni sifa aliyoyasifia Allah Muumba Mjuzi wa kila kitu matunda haya mawili. Ndani ya Aya hizi amebainisha pia watu wa aina mbili kuhusiana na matumizi ya matunda haya; wale wanaoyatumia kama chakula ambacho anakitaja hapa kama chakula kizuri na bora kabisa na kundi la pili ni la watu wanaotengeneza pombe au vinywaji vya ulevi kwa kutumia matunda haya. Jambo hili ni haramu na hapa Allah anataja tu kuwa kuna watu wanaoyafanya matunda haya kama chakula na wako wanaotengeneza pombe ambayo ni haramu kwa kutumia matunda haya. Mpenzi msomaji tende imetajwa mara nyingi katika rejea mbalimbali za Kiislamu. Imetajwa katika Qur’an, katika Hadithi za Mtume, katika Fiqhi nakadhalika. Neno ‘Pishi ya Tende’ si geni kwa wanaosoma Fiqhi ya Kiislamu liwe linaambatana na fidia za Kishariah za kulisha masikini. Wafungaji katika mwezi wa Ramadhani wanafahamu kuwa Mtume kaelekeza mfungaji anapofungua Swaumu afungue kwa tende. Hata Bi. Maryamu alipojifungua Nabii Issa Allah alimuelekeza ale tende kama chakula cha kwanza. Hata Zakatul Fitri tende inatajwa kama chakula cha kwanza katika vyakula vilivyokuwa vinatolewa Zakatul Fitri na wema waliotangulia. Kwa ujumla,tende inatajwa ndani ya Qur’ani si chini ya mara ishirini! Bila shaka kutajwa mara nyingi hivi kwa tunda hili ni ishara na dalili ya upekee wake. Mpenzi msomaji, tende ni tunda linaloongoza kwa kuliwa katika kipindi cha Mfungo Mtukufu wa Ramadhani. Tende ina ladha nzuri. Pamoja na kuwa na ladha nzuri tende imesheheni madini na vitamini kedekede na hivyo kuwa na faida nyingi sana kiafya. Miongoni mwa faida za tende kiafya; tende humpa mlaji kiasi cha kutosha cha protini na Vitamini B1, B2, B3, B5, A1, na C, virutubisho ambavyo ni muhimu kwa ustawi wa afya ya mwili wa mwanadamu. Tende huimarisha na kuboresha mfumo wa usagaji wa chakula tumboni (Digestion), hivyo humsaidia mlaji kuondokana na matatizo ya ukosefu wa choo, au matatizo ya kupata choo kigumu kinachosababisha maumivu wakati wa kujisaidia. Tende husaidia kuupatia nguvu mwili na kuuondolea uchovu, na hii ni kwa sababu tende ina virutubisho vya sukari asilia kama vile ‘glucose’, ‘sucrose’ na ‘fructose’. Vile vile, tende ina madini aina ya ‘potassium’ na kiasi kidogo cha chumvi (sodium). Madini hayo husaidia kuimarisha mishipa ya fahamu katika mwili wa mwanadamu. Pamoja na hayo tende pia huwasaidia wale wenye matatizo ya ugonjwa wa kupungukiwa damu (anemia). Vile vile inaelezwa kuwa mchanganyiko wa tende kwa viwango maalumu wa pamoja na maziwa, asali na unga wa hiliki huweza kuwa msaada kwa wale wenye shida ya nguvu za kiume. Tende vile vile huimarisha nuru ya macho na tatizo la kutokuona usiku (night blindness). Mpenzi msomaji, kuna faida nyingi za tende. Vilevile kuna tende za aina mbalimbali. Tende inaweza kuliwa kwa namna mbalimbali, kama vile kuchanganya na maziwa, kuchanganya na mkate au vitafunwa vingine. Nyumba ambayo haina tende ni nyumba ambayo watu wake w a n a n j a a h a t a k a m a wameshiba. Tende zinapatikana hapa Tanzania za kulimwa hapa hapa nchini na za kuuzwa zilizoagizwa kutoka nje hasa hasa kutoka Saudi Arabia na hata za msaada kutoka Saudia. Tujitahidi kuifanya tende kuwa sehemu ya mlo wetu wa kila siku ili tujipatie faida hizi na nyingine tusizozijua. Naam, tende ni riziki nzuri. Unajua aina ya tende inayoitwa ‘Ajuwaa? Ina jambo maalumu na la kipekee. Fuatilia makala ijayo ulifahamu jambo hilo inshaallah. Itaendelea…

Tags
Show More

Related Articles

Close
Close