4. Darasa La Wiki

Hukumu na Muongozo Sahihi Wa Mazishi Katika Uislamu

SEHEMU YA 2 Katika makala tuliishia katika kujadili hukumu za mgonjwa na mtu aliye mahututi. Katika makala hii tunaendelea kudadavua maudhui hiyo.

Mwanadamu pindi anapofikwa na mauti hana budi kuwa na subira pamoja na kuridhia maamuzi ya Allah aliyetukuka na kudura zake; na wala si vibaya kama atawafahamisha watu maradhi yake yanayomsumbua. Lakini kufanya hivyo iwe ni pamoja na kuridhia maamuzi ya Allah na kumshatakia yeye ugonjwa huo. Na mtu kutaka shifaa (uombezi) kwa Allah aliyetukuka hakumuondoshei yeye subira, bali ni Sunna na ni jambo la halali kisharia. Nabii Ayub (amani ya Allah imshukie) alimshitakia Mola wake Mlezi na kusema: “Na Ayub, alipomwita Mola wake Mlezi, akasema, ‘Mimi yamenipata madhara. Na wewe ndiye unayerehemu kuliko wote wanaorehemu,’” (Qur’an, 21:83). Na wala hakuna ubaya katika kutibu ugonjwa kwa dawa zilizokuwa halali na Mubaha. Kuna baadhi ya wanazuoni waliotilia mkazo jambo hilo hadi kukaribia daraja la wajibu. Hadithi nyingi za Mtume (rehema na amani za Allah ziwe juu yake) zimethibitisha kuchukua sababu katika kutatua mambo ikiwemo kutibiana. Kutibiana hakukinzani na suala la utegemezi wa Allah aliyetukuka, kama ambavyo pia hakupingani na uondoshaji wa njaa na kiu kwa kutumia chakula au kinywaji. Na wala hairuhusiwi kisharia kutibiana kwa njia ya haramu, kwa ushahidi wa Hadithi aliyoipokea Abuu Huraira (Allah amridhie), kwamba Mtume (rehema na amani za Allah ziwe juu yake) amesema: “Hakika Allah ndiye aliyeyaleta maradhi pamoja na dawa zake, na kila ugonjwa ameuwekea dawa, wala msitibiane kwa njia aliyoharamisha Allah aliyetukuka,”(Abuu Daudi). Na katika Sahihi Muslim imekuja kwamba Mtume (rehema na amani za Allah ziwe juu yake) amesema kuhusiana na kilevi cha pombe: “Pombe siyo dawa bali ni ugonjwa.” Kadhalika ni haramu kutibiana kwa dawa ambazo zinapingana na itikadi na imani ya Kiislamu, kama vile kufunga azima (hirizi) zilizoandikwa ndani yake michoro na maandishi ya kishirikina. Haifai pia kutibiana kwa talasimu, fingo na hirizi yoyote inayotundikwa au kufungwa katika nyumba, ofisi, shingoni na mikononi na kadhalika. Kufanya hivyo, kunaufanya moyo wa mtu uwe mbali na utegemezi wa Allah aliyetukuka na badala yake kujenga imani kwa vitu hivyo kuwa vinaleta manufaa au kuondosha madhara. Vilevile ni haramu kupeana tiba kupitia kwa makuhani, wanajimu, wachawi na watu wanaotumia majini. Njia zote hizi zilizotajwa ni za kishirikana na haifai kujitibia kupitia njia hizi kwani ni muhimu imani na itikadi ya Muislamu kubakia salama kuliko siha yake. Allah aliyetukuka amejaalia shifaa na uponyaji kupitia dawa na njia za halali ambazo zina faida kwa mwili, akili na dini. Miongoni mwa dawa hizo ni Qur’an, Kitabu cha Allah aliyetukuka kupitia njia ya kumsomea mgonjwa (Ruk’ya), pamoja na kumwombea dua zilizothibiti kisharia. Imam bin Qayyim amesema: “Na njia ya matibabu yenye tija zaidi ni kufanya amali za kheri, hisani, uletaji dhikri na dua pamoja kunyenyekea na kuleta toba. Athari ya njia hii, ina matokeo chanya kushinda dawa kutegemeana na maandalizi ya nafsi katika kuipokea njia hiyo. Na wala hakuna shida kutibiana kwa dawa za halali kupitia kwa madakatari bingwa na wenye weledi katika kuyafanyia tafiti maradhi na kuyatibu, kuanzia katika zahanati, hosipitali na kadhalika. Ni Sunna kumtazama mgonjwa Kumtazama mgonjwa na kumjulia hali yake ni Sunna na tendo lenye thawabu ndani yake, kutokana na Hadithi ya Mtume (rehema na amani ya Allah iwe juu yake) anasema kuwa: “Mambo matano ni wajibu mtu kumfanyia ndugu yake Muislamu.” Na katika mambo matano hayo, Mtume akataja kumjulia hali mgonjwa (Bukhari a Muslim). Pindi mtu anapomzuru mgonjwa anatakiwa kumwuliza hali yake. Mtume (rehema na amani ya Allah ziwe juu yake) alipokuwa akimjulia hali mgonjwa alikuwa akimsogelea na kumuuliza hali yake. Na ni vema ziara hii ya kumjulia hali mgonjwa ikawa unapumzika kila baada ya siku moja au mbili kwani mgonjwa hapendelei ziara za kila siku. Na vilevile, haifai kurefusha muda wa kumjulia hali ila itakapokuwa mgonjwa hupendelea jambo hilo. Na wewe uliyemtembelea unaweza kumwambia mgonjwa, mathalan: “Uwe na subira ndiyo hali yamwanaadamu, Allah atakuondolea tatizo lako inshaallah.” Na atajitahidi kutafuta namna ya kumfariji na kumfurahisha mgonjwa na atamuombea dua ili apone haraka na kumsomea Qur’an, hususan Surat Al-Fatiha, Ikhlasi na Muawidhatani, yaani Sura Annasi na Alfalaki.

Kurudisha amana kwa wenyewe

Ni wajibu juu ya mgonjwa kurudisha amana na haki za watu kama hilo litakuwa na wapesi juu yake. Na kama itashindikana kupitia njia hiyo, atatumia njia ya kuandika wasia katika urejeshaji wa haki na amana za watu. Kadhalika, ni Sunna mgonjwa kuusia sehemu ya theluthi moja ya mali yake kutumika katika mambo ya kheri. Hili ni jambo muhimu si kwa mgonjwa tu, bali hata kwa mtu aliye na siha timamu. Mtume(rehema na amani ya Allah iwe juu yake) amesema kuhusu uandikaji usia: “Si haki kwa Muislamu kukaa na kitu siku mbili bila ya kukiandika usia kitu hicho,”(Bukhari na Muslim). Mtume amezitaja siku mbili hapa kuonesha msisitizo tu, ila inavyotakikana mtu asikaye na mali muda wowote ule hata kama ni mchache bali aiandikie usia kwani hajui ni wakati gani mauti yatamfika. Ama katika upande wa urejeshaji haki za watu, Mtume (rehema na amani za Allah ziwe juu yake) amesema: “Mtu yeyote aliyekuwa na haki za watu, miongoni mwa heshima au mali, basi azirejesha kwa wenyewe kabla haijafika Siku ya Kiyama, ambayo mali na samani zitakuwa hazina thamani tena. Iwapo mtu huyo atakuwa na amali njema alizozifanya hapa duniani, zitachuliwa amali hizo na kupewa mdeni wake. Na kama mtu huyo hana amali njema, yatachukuliwa mabaya ya mdeni wake na kubebeshwa yeye,” (Bukhari). Na urejeshaji wa heshima ya mtu ni kwenda kumuomba msamaha. Kama hilo litazalisha chuki na uahasama, basi aende katika sehemu ambayo amemvunjia heshima mwenzake na aanze kuisafisha heshima yake. Kama hilo nalo litakuwa na uzito juu yake, basi itabidi amwoombe dua na kumtakia msamaha kwa Allah aliyetukuka. Na ama usia katika Sharia za Kiislamu unatakiwa usizidi theluthi moja ya mali, na wala hawatausiwa watu ambao wanarithi ila pale watakaporidhia warithi wengine. Na ni haramu mtu kuwanyima urithi baadhi ya watoto wake au kuwapendelea baadhi yao. Ni juu yake mtu kuusia katika kufanyiwa maandalizi ya mazishi kwa utaratibu sahihi wa Sunna, unaoafuata mafundisho na muongozo wa Mtume (rehema na amani za Allah ziwe juu yake). Vilevile, ni Sunna kuwausia watoto wako au jamaa zako wa karibu kujiepusha na mazoea ya mambo ya uzushi yanayafanywa katika mazishi ambayo si katika mafundisho ya Uislamu kwa kuifanyia kazi kauli yake Allah aliyetukuka isemayo: “Enye mlioamini! Zilindeni nafsi zenu na ahali zenu na moto ambao kuni zake ni watu na mawe,” (Qur’an, 66:6).

Tags
Show More

Related Articles

Close
Close