
Tatizo la kuandika matusi kwenye mitihani litafutiwe dawa
Tatizo la baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kuandika lugha za matusi kwenye mitihani ya kitaifa limekuwa likijitokeza mara kwa mara hapa nchini. Baraza la Taifa la Mitihani (Necta) limekuwa likikemea tabia hii na kuchukua hatua kadhaa ikiwemo kuwafutia matokeo wanafunzi walioandika matusi kwa mujibu wa sheria za baraza hilo.
Hata hivyo, adhabu hiyo inaonekana kushindwa kufua dafu, kwani kila mwaka tatizo hili limekuwa likijirudia. Kwa mfano, wiki iliyopita Necta ilifuta matokeo ya watahiniwa 67 wakiwemo watano walioandika matusi katika mtihani wa Taifa wa kidato cha nne uliofanyika mwezi Novemba mwaka jana.
Pia, mwaka jana Necta ilifuta matokeo ya watahiniwa 61 wa darasa la saba kutokana na udanganyifu na kuandika matusi.
Kutokana na kushamiri kwa tabia hii, Katibu Mtendaji wa Necta, Dkt. Said Mohammed amesema, pamoja na kufuta matokeo ya wanafunzi walioandika lugha za matusi kwenye mitihani ya kidato cha nne, pia wameziandikia barua shule walizosoma ili kutoa taarifa kwa wazazi wao wawachukulie hatua za kimaadili kwa kuandika matusi.
Dkt. Mohammed amesema, kuandika matusi kunaendana na suala la maadili si kwenye mitihani tu bali mahali popote, hivyo matusi hayakubaliki mahali popote.
Zipo sababu lukuki zinazotajwa kuchangia baadhi ya wanafunzi kuandika matusi kwenye mitihani yao ikiwemo suala zima la mmomonyoko wa maadili.
Mmoja wa walimu alinukuliwa akisema kuwa tatizo la wanafunzi kuandika matusi hujitokeza pia hata katika mitihani ya ndani kutokana na wanafunzi hao kutopenda shule huku pia kukiwa na mmomonyoko wa maadili unaosababisha wanafunzi kujifunza lugha za matusi.
“Hakuna mwanafunzi ambaye amejipanga kufaulu akaandika matusi kwenye mtihani, hao wanaoandika matusi unakuta hawana maandalizi na wengine hata mahudhurio yao huwa ni hafifu,” alisema mwalimu huyo alipokuwa akihojiwa na chombo kimoja cha habari hapa nchini.
Kwa hali hii yawezekana kabisa pia baadhi ya wanafunzi, hususani wanaosoma shule za kutwa wanajifunza matusi na lugha za mtaani kutokana na kuchanganyika na jamii za huko. Matokeo yake wanaingia kwenye vyumba vya mitihani huku vichwa vyao vimejaa mambo mengi yasiyo na maadili.
Ni jambo la kutia moyo kwamba idadi ya wanafunzi wanaoandika matusi kwenye mitihani ya kitaifa ni ndogo na inaweza kushughulikiwa ikiwa kutakuwa na ushirikiano kati ya wazazi na walimu. Sasa ili kufikia malengo ya kumaliza tatizo hili, kwanza tunashauri wazazi wakae na watoto wao na kuwaeleza faida na umuhimu wa elimu katika maisha yao.
Wazazi na walimu wana jukumu la kuwaambia watoto kwanini wapo shule tangu wakiwa darasa la kwanza ili wazingatie masomo na kufaulu vizuri. Pia, Baraza la Mitihani (Necta) litoe elimu katika shule na vituo vya mitihani ambapo watahiniwa wanatokea.
Fauka ya hayo, pia tunashauri mamlaka husika ziendelee kuchunguza kwa undani kadhia hii na kuwachukulia hatua za kisheria wazazi watakaobainika kuwashawishi watoto wao kuandika lugha za matusi kwenye karatasi za mitihani.
Tunasema hivyo kutokana na ukweli kwamba, ripoti nyingi zinaonesha wazazi wengi wanaowashawishi watoto wao kuandika matusi kwenye mitihani ya kitaifa wanafanya hivyo ili wasiendelee na masomo na badala yake wawaoze au wawasaidie kufanya kazi za kilimo, kuchunga mifugo, au kufanya mambo mengine yenye maslahi kwao.