
Mafunzo ya msingi kutoka moto wa Los Angeles – (Sehemu ya mwisho)
Katika makala iliyopita tulimalizia na ushauri kwa waumini juu ya kumrejea Allah, kumuomba msamaha na kufikiria aina gani ya madhambi tuliyofanya ili tuweze kutubu. Sasa tumalizie sehemu ya mwisho ya makala haya.
Aina tofauti za matarajio
Ni kweli kwamba Allah ‘Azza wa Jallah’ anataka majibu zaidi kutoka kwa wasio Waislamu, kwa sababu hawajajisalimisha kwake. Waislamu, ambao tayari wameshajisalimisha kwake, Allah anawataka watubu.
Allah anawataka wale wote walioathiriwa na majanga kutubu na kutafakari kupitia majanga hayo. Wasio Waislamu wanapaswa hatimaye kuukumbatia Uislamu, na Waislamu wanapaswa kuachana na madhambi na kurejea kwake.
Waislamu, pia ni lazima waendelee kutayarisha na kutafuta nguvu za kuwashinda maadui zao bila ya kujali majanga ambayo Mwenyezi Mungu anayaleta duniani. Hatupaswi kutegemea adhabu zake ili tupige hatua dhidi ya maadui zetu.
Majanga hutokea kwa sababu ya kiburi
Kwa kiasi kikubwa, Allah ‘Azza wa Jallah’ analeta majanga kwa watu pale wanapofanya udhalimu, na hususani wakati wanapoonesha kiburi. Mwenyezi Mungu anaona madhambi yanayotendwa na watu, lakini wakati mwingine anachelewesha kuleta majanga ili watu hao waweze kurejea kwake.
Lakini, Mwenyezi Mungu anakasirika sana anapoona watu wanaonesha kiburi na kufanya dhuluma dhidi ya wengine, kwa hiyo anawaletea adhabu. Na ndiyo maana Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Hakuna dhambi inayostahiki zaidi kuadhibiwa na Mwenyezi Mungu kwa mwenye kuitenda katika dunia hii, pamoja na yale anayomuwekea katika ulimwengu ujao, kuliko dhuluma na kukata uhusiano.” [Sunan Abi Daudi].
Kwanini Waislamu wanapatwa na majanga
Ndani ya Qur’an, Allah ‘Azza wa Jallah’ anawazungumzia watu ambao waliangamizwa kutokana na madhambi yao. Kwa mfano, Allah anasema: “Na hivyo ndivyo inavyokuwa Mola wako anapoikamata miji inapokuwa imedhulumu. Hakika mkamato wake ni mchungu na mkali.” [Qur’an, 11:102].
“Na kwa yakini tumeziangamiza kaumu za kabla yenu walipodhulumu, na waliwajia Mitume wao kwa Ishara zilizo wazi, lakini hawakuwa wenye kuamini. Ndiyo kama hivyo tunavyowalipa watu wakosefu.” [Qur’an, 10:13].
Ni kweli kwamba aya hizo zinayazungumzia mataifa yaliyopita, lakini kanuni ya kiungu bado ipo na inaweza kutumika hata kwetu. Mataifa yaliyopita yalifutwa kabisa, lakini umma wa Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) hautakuwa na hatima sawa kama hao. Lakini kutakuwa na viwango fulani vya maangamizi katika sehemu fulani fulani.
Bila shaka kunapokuwa na majanga, watu wasio na hatia wataathirika, lakini kama Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alivyosema kuwa watafufuliwa kulingana na nia zao.
Allah huwaadhibu madhalimu kwa muda autakao
Serikali ya Shirikisho ya Marekani imekuwa ikionesha kiburi na kufanya dhuluma kubwa. Watu wamekuwa wakisubiri kuona Allah ‘Azza wa Jallah’ nini atawafanya madhalimu hawa. Wengi hujiuliza, “Hivi Mwenyezi Mungu hayaoni haya?”
Bila shaka anayaona sana, ila tu kama anavyotuambia mwenyewe ndani ya Qur’an kuwa, anawacheleweshea adhabu ili waweze kurejea kwake. Lakini katika hali fulani, Mwenyezi Mungu havumilii dhuluma hii na kiburi, hususani kama kile kinachooneshwa na serikali ya Marekani kwa kuipa silaha Israel kwa ajili ya kuwaua watu wasio na hatia wa Gaza.
Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Hakika Mwenyezi Mungu huwapa muda madhalimu. Lakini anapomshika, hamuwachi kutoroka.” [Bukhari na Muslim]. Mwenyezi Mungu anajua zaidi wakati, jinsi, na kiwango kinachofaa cha kuwashughulikia madhalimu.
Kiburi cha Donald Trump
Kiburi kilichooneshwa na Rais Donald Trump wakati ule kabla hata hajaapishwa kuwa Rais ni kibaya sana kuliko hata utawala uliopita. Januari 7, 2025, siku ambayo moto wa nyika ulianza jijini Los Angeles, Trump alisema iwapo watu wa Gaza hawatasalimu amri kwa kile anachotaka, basi ‘Jehannam’ itawaka katika ukanda mzima wa Mashariki ya Kati. SubhanaAllah!
Kwa kuakisi Qur’an na Sunna, tunaweza kuona kwamba Allah ‘Azza wa Jallah’ amemuonesha Trump kwamba Yeye ndiye Mmiliki wa Moto wa Jehannam, na amemuonesha Trump kwamba Yeye ndiye anayeweza kusababisha moto duniani.
Mwenyezi Mungu angeliweza kuleta majanga mengine, lakini kama alivyosema Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) kwamba:”….hakuna anayeadhibu kwa moto isipokuwa Mola wa moto.” [Sunnan Abi Daudi].
Ni ukweli usiopingika kwamba janga hili la mto limewafanya Wamarekani wasio Waislamu waanze kutafakari sera kandamizi na dhuluma za serikali yao ya shirikisho, hususani kuhusiana na Gaza. Baadhi yao tayari wameunganisha moja kwa moja suala la Gaza na moto huo wa nyika, wakizingatia zaidi hatua ya Marekani kusaidia na kufadhili utawala dhalimu wa Kizayuni. Kwa kuongezea, kuna habari zinazozunguka kwamba, makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya utawala wa Israel na upinzani uliopo Gaza, ni kwa sababu baada ya moto huu wa nyika ulioleta uharibifu mkubwa, Marekani haina tena utulivu wa kiuchumi kuwaunga mkono.